Habel Chidawali, Singida
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa jana alitoa kile kilichokuwa kikimsibu moyoni mwake kwa muda mrefu na kusema kuwa atashinda vita dhidi yake.
Akitumia vifungu vingi vya Biblia, Lowassa ambaye amekuwa katika misukosuko mingi ya kisiasa tangu alipojiuzulu Februari 2008, alisema kuwa sasa yamekwisha baada ya kuvumilia kwa muda mrefu sana huku akisemwa maneno ya ovyo.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Amani mjini hapa.
“Wamesema maneno mengi ya ovyo sana juu yangu lakini nilivumilia siasa hizo kwa kiasi kikubwa sana hadi leo nimesimama katika imani na bila shaka nitashinda,’’ alisema Lowassa na kushangiliwa na umati wa waumini waliohudhuria.
Kauli ya Lowassa imekuja siku tatu baada ya kutoa ya moyoni kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kuhusu kile alichosema kuwa ni baadhi ya viongozi wa chama kutumia fedha nyingi kuzunguka nchini na kumtukana ovyo.
“Mwenyekiti kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama wakinitukana, hivi hatukujua kwamba kuna kamati hizo za maadili,” Lowassa alinukuliwa akihoji baada ya NEC kuridhia ombi la Kamati Kuu ya chama hicho (CC) kwamba suala la mageuzi ndani ya CCM maarufu kama kujivua gamba lirejeshwe katika kamati hiyo ili lifanyiwe kazi kwa taratibu za kawaida za kinidhamu baada ya wahusika kukataa kuachia nafasi zao.
Katika kikao hicho, Lowassa alinukuliwa akiwataja Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara, John Chiligati kwamba wamekuwa wakitukana watu ovyo kwa fedha wanazopewa na CCM.
Jana akihutubia katika hafla ya kuchangia usharika huo, Lowassa alisema: “Siku moja nilikuwa nyumbani na mke wangu tukiangalia televisheni... katika kipindi cha uchambuzi wa magazeti tukakutana na habari ambayo hata wachambuzi wa magazeti wenyewe walishindwa kuisoma kutokana na mambo mabaya ambayo yaliandikwa juu yangu.’’
Alisema mke wake alichukua Biblia na kusoma katika kitabu cha Isaya sura ya 41 mstari wa 10 na kisha akamtia moyo na kumfanya avumilie kwa kipindi chote cha misukosuko hiyo huku akimuomba Mungu.
Maneno katika kitabu hicho yanasomeka: “Usiogope kwa maana mimi ni pamoja nawe, usifadhaike kwa maana mimi ni Mungu wako nitakutia nguvu, nitakusaidia na kukushika mkono wa kuume wa haki yangu.’’
Lowassa alisema kuwa katika kipindi chote hicho amekuwa akiishi kwa matumaini ya neno hilo lililosomwa na mke wake na hata yalipokuwa yakisemwa maneno mengi juu yake aliamini kuwa yote yatapita kwa kuwa yalilenga kumchafua tu na hayakuwa na ukweli ndani yake.
Alitumia pia maneno ya Biblia katika kitabu cha Warumi 8:31 ambayo yanasema: “Basi tuseme nini juu ya hayo, Mungu akiwapo upande wetu ni nani aliye juu yetu.’’
Tofauti na alivyokuwa akionekana baada ya kujiuzulu, Lowassa jana alikuwa mwenye furaha zaidi akionyesha ujasiri wakati wote wa shughuli hiyo ya uchangiaji ambayo alisimama kwa zaidi ya saa nne akichangisha fedha za ujenzi wa kanisa hilo.
Awali, ilitarajiwa kwamba kiasi cha Sh100 milioni tu ndicho kingechangishwa katika hafla hiyo lakini lengo hilo lilivukwa na kupatikana Sh138 milioni. Lowassa alichangia Sh10 milioni.
Mbunge huyo alisema kuwa kila jambo linalomjia binadamu huwa ni la muda na baada ya hapo ukweli huonekana mbele yake na hivyo akawasihi Watanzania kuwa wavumilivu juu yake na maisha yao kwa ujumla.
“Nawashukuru sana mashehe, viongozi wa dini, wana maombi, wake kwa waume, pamoja na viongozi mbalimbali bila ya kuwasahau marafiki zangu ambao kwa namna moja au nyingine walifunga kwa maombi juu yangu, nasema asanteni sana.’’
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Kati, Eliufoo Sima alisema hata kama mawingu yatapita juu ya jua, haina maana kuwa jua limekwisha.
“Tunakutia moyo kwamba wale waliosema kuwa mapambano katika maisha hayatakwisha na suluhisho si kuyaogopa, bali kuyatafutia jawabu kwa upole, hekima na utulivu,’’ alisema Askofu Sima.
Alisema kuwa wanadamu wamezoea kushangilia maovu siku zote lakini umefika wakati ambao wanatakiwa kushangilia hata kwa mema pia ikiwemo masuala ya utoaji michango kwa ajili ya masikini na walio na mahitaji.
Akitumia maneno kutoka katika Biblia, Askofu Sima alimtaka Lowassa kutokata tamaa katika utumishi wake.
No comments:
Post a Comment