Thursday, November 17, 2011

Syria ina siku tatu kumaliza ghasia

Jumuiya ya nchi za kiarabu imeipa Syria siku tatu kumaliza mzozo unaoendelea nchini humo la sivyo itawekewa vikwazo vya kiuchumi.
Habari kutoka Damascus zinasema majeshi yalioasi yameendelea kulenga kambi za jeshi linalotii serikali.
Ni miezi minane ambapo waandamanaji wasiokuwa na silaha wamekuwa wakilengwa na wanajeshi watiifu kwa Rais Bashar Assad.
Hali imebadilika sasa na majeshi yalioasi yameanza kukabiliana na mahasimu wao.
Naye waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Alain Juppe anatarajiwa kufanya ziara maalum nchini Uturuki, kujadili hatua dhidi ya mzozo unaoendelea nchini Syria.
Duru zinasema kwamba majeshi yalioasi wanaojiita Jeshi Huru La Syria, yameshambulia vituo kadhaa vya kijeshi mjini Damascus na kuwaua wanajeshi kadhaa wa serikali ya Syria, hata hivyo madai hayo bado hayajathibitishwa.
Lakini ikiwa madai haya yana ukweli wowote, basi ni ishara kwamba huenda mzozo wa Syria umechukua mkondo hatari.
Jumuiya ya nchi za kiarabu imeonya kuiwekea Syria vikwazo vya kiuchumi ikiwa serikali ya Rais Assad haitakoma kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji na imetaka dhuluma hizo kukomeshwa katika kipindi cha siku tatu zijazo.
Ututruki pia inatathmini kuiwekea Syria vikwazo. Tayari Marekani na jumuiya ya Ulaya zimeweka vikwazo, japo haijabainika athari za vikwazo hivi ni zipi.
Nchi za magharibi zimeanza kutafakari mustakabali wa Syria bila uwongozi wa Bashar Al Asaad.
Hata hivyo pande zote ziko makini kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment