Thursday, November 17, 2011

Kisa na mkasa na Salim Kikeke

Kula ukiwa umevaa nguo

Moja ya jiji linalotajwa kuwa huru na lenye uvumulivu nchini Marekani, San Fransisco, sasa limeamua kuweka bayana kuhusu suala la watu kula chakula hadharani wakiwa hawajavaa nguo.
Bodi ya wasimamizi ya jiji hilo imeweka sheria mpya kukataza watu wasiovaa nguo kula katika migahawa, bila kufunika na vitambaa viti wanayokalia, limeripoti gazeti la San Fransisco Examiner.
Yeyote atakayekiuka sheria hiyo mpya atapigwa faini ya dola mia moja kwa mara ya kwanza, na dola mia mbili iwapo watarudia tena, na mara ya tatu atapigwa faini ya dola elfu moja au kwenda jela kwa mwaka mmoja. Watu kutembea bila nguo mitaani ni jambo linalovumilika mjini humo hasa katika eneo la Castro.

FLAT SCREEN GEREZANI


Polisi mjini Acapulco kusini magharibi mwa Mexico wamekuta wafungwa katika gereza moja wakiwa na televisheni mia moja, deki za DVD, magunia mawili ya bangi na majogoo mia moja.
Polisi wamesema televisheni hizo zilikuwa flat screen. Aidha wamesema wamekuta pia wanawake 25 wakiishi katika sehemu ya wafungwa wanaume, sita kati yao walikuwa wafungwa, lakini 19 waliosalia ni wahamiaji haramu, ambao vyombo vya habari vimeripoti kuwa ni makahaba.
"Hatimaye tumekamata wanawake 25 wakiwa wamevaa mawigi" Amesema Arturo Martinez, msemaji wa jimbo la Guerro. Majogoo mia moja waliokutwa ndani ya gereza hilo imeelezwa ni kwa ajili ya mchezo wa kuwapiganisha ambao ni maarufu katika eneo la Amerika ya Kusini.
Mkuu wa gereza hilo, mkuu wa usalama wa gereza na baadhi ya walinzi wa gereza hilo wamefukuzwa kazi.

111111

Kimamama waja wazito wanaokaribia kujifungua nchini Korea Kusini, walipeleka maombi ya kutaka kujifungua kwa kufanyiwa upasuaji siku ya Ijumaa, ili watoto wao wazaliwe, tarehe kumi na moja ya mwezi wa kumi na moja mwaka elfu mbili na kumi na moja.
Namba za utambulisho wa utaifa wa Korea Kusini zina tarakimu kumi na tatu, na tarakimu sita za mwanzo huwa tarehe ya kuzaliwa, na hivyo vitambulisho vya watoto hao vitakuwa na vikianza na namba 111111 na kufuatiwa na namba nyinginezo. Idadi ya kinamama waliotaka kujifungua mwaka huu ni asilimia 20 zaidi ya miaka mingine.
Kinamama ambao tarehe zao za kujifungua ni wiki moja baada ya tarehe kumi na moja wamesema wako tayari kujifungua mapema, limeripoti gazeti la Seoul. Wakati huohuo, mapacha wawili nchini Marekani walipanga kufanya sherehe kubwa ya kuadhimia miaka kumi na moja ya kuzaliwa, siku ya tarehe kumi na moja mwezi wa kumi na moja mwaka 2011.
Novemba kumi na moja ni maarufu nchini Korea Kusini ikijulikana kama siku ya Pepero, au siku tamu, sawasawa na siku ya wapendanao ya Valentine.

NYUKI

Zaidi ya nyuki elfu sitini wamekutwa katikia myumba ya bwana mmoja aliyekutwa amekufa nchini Marekani.
Mtandao wa news.com umesea bwana huyo amekufa kutokana na sababu zosizojulikana, lakini nyuki walikutwa wakiinshi ndani ya ukuta wa nyumba yake.
Mtu huyo ambaye hakuwa ametambuliwa alikutwa na mwanaye wa kike, kimeripoti kituo cha TV cha WPLG. Mtaalam wa nyuki Willie Sklaroff ambaye ataondoa nyuki hao amesema wako karibu elfu sitini.
Taarifa zinasema bwana huyo alikuwa akikarabati nyumba hiyo kwa ajili ya kumpa mwanaye wa kike, lakini pia haifahamiki kama alikuwa akiwafuga nyuki hao, au hata kama alikuwa akifahamu kama wanaishi nyumba moja.

KADI NYEKUNDU KWA KUVAA NYEKUNDU

Mwamuzi mmoja wa soka hapa Uingereza alitoa kadi nyekundu kwa wachezaji sita kwa sababu ya rangi ya nguo zao za ndani.
Tukio hilo liliokea Wales ambapo mwamuzi aligundua mchezaji wa timu moja alikuwa amevaa nguo nyeupe ya ndani huku bukta yake ikiwa rangi nyekundu, limeripoti gazeti la Bath Cronicle.
Mchezaji mwingine alionekana na mwamuzi huyo akiwa kavaa nguo ya ndani ya rangi nyeusi. Mchezo huo ulikuwa kati ya timu moja ya England ikipambana na Bath City ya Wales.
Sheria za chama cha soka cha England zinasema wachezaji wanatakiwa wavae rangi zinazifanana za nguo za ndani na nje. Hata hivyo sheria hiyo huwa haizingatiwi sana.
Kuongeza utata, refa huyo aliwataka wachezaji wawili kubadili nguo zao mbele ya mashabiki, na wakati wawili hao wako nje, timu yao ikafungwa bao moja.
Timu hiyo iliishia kuchapwa mabao 6 kwa bila.

Na kwa taarifa yako...

Chuma huwa kizito zaidi kikipata kutu.
Tukutane wiki ijayo... Panapo majaaliwa...

No comments:

Post a Comment