Thursday, November 17, 2011

EU, Marekani wajitosa mgogoro wa Katiba

WAKUTANA NA OFISI YA SPIKA, UPINZANI BUNGENI DODOMA
MVUTANO baina ya wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi kwa upande mmoja dhidi ya Serikali na wabunge wa CCM kwa upande mwingine, umevuta nchi wahisani ambao wametuma maofisa wake mjini Dodoma kuchunguza kiini cha mvutano uliopo. Ujumbe wa maofisa watano ukiongozwa na Balozi wa Sweden nchini, Lennart Hjelmaker ulifika katika Ofisi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na baadaye kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila.
Imeelezwa kwamba ujumbe huo wa nchi ambazo ni wafadhili wa Tanzania, umehoji masuala mbalimbali kuhusu mchakato unaoanza sasa wa kuiwezesha Tanzania kupata Katiba Mpya.

Taarifa hizo zinasema, maofisa hao wengi wakiwa ni wale wanaohusika na ushauri wa masuala ya siasa katika balozi hizo, wamekuwa wakihoji hatima ya msimamo wa upinzani ambao waliamua kususia Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.
Chana akizungumza na kwa simu jana alikiri kukutana na ujumbe huo ambao pia uliwajumuisha maofisa kutoka balozi zilizopo kwenye mabano, Logan Wheeler (Marekani), Veslemoy Lothe Salvessen (Norway), Mark Polatjko (Uingereza) na Dk Carol McQueen (Canada).
Maofisa hao wakiambatana na wengine kadhaa, jana asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu Bungeni, walitambulishwa na mmoja wa wenyeviti wa Bunge, Janister Mhagama wakiwa kwenye Ukumbi wa Spika.

Chana jana alisema: “Ndiyo nilikutana nao na walichotaka kufahamu tu ni jinsi mchakato mzima wa sheria hii ulivyokwenda na hatua zote tulizopitia kama kamati hadi kufikishwa kwake bungeni.

Alipoulizwa iwapo walihoji suala la Wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi kususia mjadala wa muswada huo, Mwenyekiti huyo alijibu kwa kifupi tu: “Ndiyo, hata hilo walitaka kufahamu lilivyokuwa.”
Imeelezwa pia kwamba ujumbe huo ulifika Ofisini kwa Spika Makinda, lakini haikufahamika mara moja kama walipata nafasi ya kuzungumza na kiongozi huyo wa Bunge, kutokana na jana kutokuwepo ofisini.

Wabunge wa upinzani
Juzi usiku, ujumbe huo ukiongozwa na Balozi Hjelmaker ulikutana na Lissu pamoja na mambo mengine ukihoji sababu za kutoka nje ya ukumbi wa bunge.
Ujumbe huo pia ulihoji hatua ambazo wapinzani hao wanakusudia kuchukua ikiwa Bunge litatumia wingi wa wabunge wa chama tawala kupitisha muswada huo, kisha kupata baraka za Rais na kuwa sheria ya nchi.
Pia walihoji iwapo kuna dalili zozote za kufanya mazungumzo ya kuwezesha pande husika kufikia mwafaka wa pamoja, ili wote waweze kushiriki katika mchakato wa kuwezesha nchi kupata Katiba Mpya.

Akizungumzia kukutana ujumbe huo Lissu alisema: “Ndiyo, nimekutana nao na wamehoji mambo mengi kwelikweli lakini niseme kwamba inavyoonekana wana hofu kuhusu investiment (uwekezaji) ikiwa hakutakuwa na makubaliano.”
“Nimewaambia kwamba sisi msimamo wetu ni kwenda kwenye mahakama ya wananchi, kuwaambia kwamba tumekataa kuhalalisha mchakato haramu wa upatikanaji wa Sheria maana tangu mwanzo kanuni na sheria za nchi zilikiukwa.”
Kwa upande wake, Kafulila pia alikiri kukutana na ujumbe huo jana, bila kuwapo kwa Balozi wa Sweden ambaye aliondoka Dodoma kurejea Dar es Salaam, baada ya kipindi cha maswali na majibu.

“Kwangu ni kama walitaka kufahamu kuhusu mambo matatu, kwanza kwa nini tuliamua kutoka nje, nilivyotumia nafasi yangu ndani ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala nilipoteuliwa na Spika kuingia kwenye kamati hiyo na nini kinafuata ikiwa muswada huo utapitishwa na baadaye kuwa Sheria,” alisema Kafulila na kuongeza:

“Kwa kifupi nimewaambia kwamba sababu za kuondoka ziko wazi na tumezisema mara nyingi, lakini kubwa nimewaambia kwamba mimi mawazo yangu ni kuwahamasisha wanaharakati na hata wabunge wenzangu wa Chadema kuona kama tunakuwa na mchakato wetu, sambamba na ule unaofanywa na Serikali.”
Kafulila alisema mchakato huo utawawezesha wanaopinga wa Serikali kuwa na mfano wa bora na kwamba matokeo ya kazi hiyo, yatatumika kuushawishi umma wa Watanzania kupiga kura ya hapana dhidi ya Katiba ‘haramu’, inayokusudiwa kutungwa kutokana na mfumo ‘haramu’.

Siku za mjadala zaongezwa
Mjadala kuhusu muswada huo uliendelea jana na umeongezewa siku hadi leo utakapohitimishwa majira ya mchana.Habari zilizopatikana zinasema kuongezwa kwa muda wa majadiliano kunaweza kuathiri ratiba ya Bunge na kwamba upo uwezekano wa kuongezwa kwa siku moja ili Bunge liahirishwe Jumamosi.
Mkutano wa Tano wa Bunge, bado unakabiliwa na kazi ya kujadili muswada mmoja wa sheria na kupokea taarifa mbili za kamati ambazo kimsingi zinaweza kuhitaji kujadiliwa.

Taarifa hizo ni ile ya Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa akichunguza tuhuma za Wizara za Serikali kuchangisha fedha kutoka katika taasisi zilizoko chini yake kwa lengo la kupitisha bajeti bungeni na ile ya Kamati ya Nishati na Madini kuhusu sekta ya gesi nchini.

Mashambulizi kwa upinzani
Jana,  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira aliungana na Mawaziri Profesa Anna Tibaijuka wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu kuchangia muswada huo na kutuhumu kauli zilizotolewa na Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, Tundu Lissu akisema ni mpotoshaji.

Wassira alisema anakishangaa Chadema kwani wakati wanagombea Urais mwaka 2010, walisema “Wakichukua tu madaraka nchi hii watahakikisha wanatubadilishia katiba ndani ya siku 100 lakini sasa hivi wanabadilika tena wanasema haraka ya nini.”

Alisema hata wasomi na wanaharakati nao pia wanawapotosha wananchi kwa kusema mambo yasiyo ya kweli kuhusu mchakato huo. Alisema wasomi wanadai kwamba Bunge linatunga Katiba wakati wanajua halina mamlaka hayo, badala yake wanatakiwa kupelekewa wananchi waipitie na kutoa maoni yao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge alisema kuna kundi la watu linapotosha wananchi kwa kujiona wao wanachokitaka lazima kiwe hivyo hivyo. Chenge ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema kundi hilo linashinikiza wananchi kufuata maoni yao kwa sababu limejiaminisha kwamba wao pekee ndiyo wanaoweza kutoa maoni yao yakasikilizwa na zaidi ya Watanzania 40.

Naye Agripina Buyogela Kasulu Vijijini (NCCR), alisema  mchakato wa huo ufuate haki kwa kufuata hekima za Mwalimu Julius Nyerere wakati wa mchakato wa kura za maoni kuhusu vyama vingi. Alisema asilimia 80 ilikataa vyama vingi lakini asilimia 20 ilikubali lakini kutokana na hekima za Mwalimu ilibidi akubali kura za watu wachache, ndiyo maana mpaka leo kuna vyama vingi.

Muswada huo umekuwa ikipingwa na wasomi kupelekwa bungeni kujadiliwa badala yake wakitaka urejeshwe kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma ya Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji alisema unatakiwa kusomwa kwa mara ya kwanza. Alipendekeza Tume ya Katiba kuwa na wataalamu wasiozidi 20 badala ya 30, kwani idadi hiyo ni kubwa mno akitaka pia majina ya wanaotakiwa kuiunda wapendekezwe na vyuo vikuu na vyama vya kitaaluma na Rais ateue majina kutokana na mapendekezo hayo.

Nahodha aonya
Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata wote wanaotishia hali ya amani kwa kutangaza kuitisha maandamano bila kikomo.

Nahodha alisema jeshi hilo linatakiwa kuchukua hatua hiyo ya kuwakamata wanaotishia usalama wa raia kwa kutoa maneno ya uchochezi kwa wananchi ya kuandamana kuhusu katiba kwani ni kosa.

Wakati Nahodha akisema hayo, Baraza la Vijana la Taifa la Chadema (Bavicha), kupitia kwa Mwenyekiti wake, John Heche limetangaza kufanya maandamano katika majimbo ya wabunge wote watakaounga mkono muswada huo.Habari hii imeandaliwa na Neville Meena, Dodoma Keneth Goliama, Hussein Issa na Geofrey Nyang'oro, Dar

No comments:

Post a Comment