Saturday, November 19, 2011

JK kuteta na wabunge wanachama wa TAPAC leo Dom

Na Godfrey Ismaely, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete, anatarajia kuwa
ngeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya Umoja wa
Wabunge wa Tanzania wa Kupambana na Ukimwi (TAPAC) utakaofanyika katika
ukumbi wa zamani wa bunge maarufu kama ukumbi wa Pius Msekwa leo.


Taarifa ya ujio wa Rais ilitolewa jana Mwenyekiti wa TAPAC Bi. Lediana
Mng’ong’o, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

Alisema lengo la maadhimisho hayo ni kutimiza miaka 10 tangu
kuzinduliwa kwake mwezi Novemba mwaka 2001.

Alisema umoja huo ulianzishwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuunganisha nguvu katika vita dhidi
ugonjwa wa UKIMWI nchini ikiwemo katika majimbo wanakotoka wawakilishi hao wa wananchi.

Alisema umoja huo unajihusisha katika kutetea na kulinda haki za
watu wanaoishi na Virusi vya UUKIMWI (VVU) na walioathiriwa na ugonjwa huo.

Bi. Mng’ong’o alisema umoja huo pia unashiriki kikamilifu katika kutunga
sheria za kuongeza rasilimali kwa ajili ya kuwaudumia watu wanaoishi na
VVU nchini.

Mbunge huyo alisema maadhimisho hayo yataambatana na kongamano la tano
na mkutano wa mwaka utakaoendelea leo na Jumapili katika ukumbi huohuo wa Pius Msekwa.

No comments:

Post a Comment