Wednesday, November 23, 2011

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Pombe kukamata wezi

Bia
Bia yavutia wezi kujisalimisha
Polisi duniani wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kujaribu kuwakamata wahalifu wanaosakwa, lakini hapa Uingereza polisi wamewaomba wezi wanaotafutwa kujisalimisha wenyewe na wakifanya hivyo watapatiwa bia za bure.
Polisi katika jimbo la Derbyshire wametoa fursa hiyo kwa kundi la washukiwa kadhaa, ambao wameahidiwa watapewa creti moja la bia kwa kila atakayejisalimisha.
Kampeni hiyo ya polisi inayojulikana kama Operation Rocky tayari imewavutia washikiwa kumi na tisa, ambao wamejisalimisha na kukata kiu zao za bia. "Hawa ni wahalifu ambao wamekuwa wakiukimbia mkono wa sheria kwa muda mrefu, kwa hiyo tumeamua kutumia njia hii" amesema inspekta mkuu Graham McLaughlin. Washukiwa hao wanatafutwa kwa uhalifu wa wizi na kunyanyasa kijinsia.

Wivu

Dem
Wivu waleta matata
Mwanamama mmoja aliyekuwa akihisi kuwa mumewe ana mwanamke mwingine, alisababisha mtafaruku baada ya mwanaume huyo kukuta kifaa kwenye gari lake na kudhani ni bomu.
Bwana huyo, mfanyabiashara aitwaye William Sachiti aliona kifaa kisicho cha kawaida kwenye gari lake na kuhisi labda ni bomu lililotegwa na mahasimu wake wa kibiahara. Bwana huyo alipiga simu mara moja polisi na kikosi maalum cha kutegua mabomu kuitwa na kusababisha mtaa mzima kufungwa, katika eneo la Surrey hapa London.
Bwana huyo alipompigia kewe simu kuwa kuna bomu limetegwa garini mwake, mke huyo aliomba radhi mara moja na kusema, aliagiza mtu aweke kifaa maalum kitachoweza kutazama nyendo za mumewe kila aendapo.
Kifaa hicho kinaitwa GPS. "Naomba sana radhi, Nadhani ni wivu tu" amesema mke huyo. Kikosi cha kutegua mabomu, idara ya zima moto na magari ya kunebebea wagonjwa yalikuwa yamekusanyika kufuatia sakata hilo wakidhani kutakuwa na mlipuko kubwa.

Kinyozi mjanja

Kinyozi
Amua mwenyewe ulipe ngapi

Kinyozi mmoja nchini Marekani ambaye kwa miaka ishirini amekuwa akikodisha viti kuendesha biashara hiyo, hatimaye amepata mtaji wa kununua vifaa vyake mwenyewe, lakini sasa mtikisoko wa uchumi unamtikisa.
Watu wengi katika kubana matumizi wameacha kukata nywele. "Yaani hiyo ni moja kati ya mambo ya mwanzo ya kubana matumizi" amesema kinyozi hyo, Gregory Burnett mjini Canton, Ohio. Kupambana na hali hiyo, miezi miwli iliyopita kinyozi huyo alibandika tangazo kuwaambia wateja walipe kiasi wanachoweza.
"Hali ni ngumu" limesema tangazo hilo "Kwa hiyo utalipa kiasi unachotaka wewe mteja" limalizia tangazo hilo mbele ya duka la kinyozi huyo liitwalo Old School.
Tangu aweke tangazo hilo watu wameanza kumiminika kwenda kukata nywele. Kwa miaka miwili Burnett amekuwa akitoza dola kumi na mbili kukata nywele, lakini sasa anafikia kuchukua hata dola tano. "Nawaambia wateja kuwa kukata nywele ni bure, hizo utakazolipa ni ada ya kukalia kiti" amesema Burnett. Mbali na mpango wake huo, pia anawaahidi wateja kuwapa mazungumzo ya kuvutia katika kipindi chote atakachokuwa akiwakata nywele.

Mwizi na Krismasi

Christmas
Mapambo ya Krismasi
Mwizi mmoja nchini Marekani amevunja nyumba ya watu, na kisha kuanza kuweka mapambo ya sherehe za krismasi ndani ya nyumba hiyo.
Mwizi huyo wa Vandalia, Ohio alivunja nyumba na kuingia wakati wenye nyumba hiyo hawapo, na kisha kuanza kupamba nyumba hiyo. Polisi wa huko waliokaririwa na kituo cha televisheni cha WHIO wamesema mtoto mwenye umri wa miaka 11 aliporejea nyumbani kwao na alimkuta mwizi huyo akiwa amekaa juu ya kochi huku akitazama TV.
Kijana huyo mara moja alimuita mama yake, ambaye aliwataarifu polisi. Mishumaa ilikuwa imewashwa, TV ilikuwa imefunguliwa kwa sauti ya juu, na mapambo kila mahala" amesema mama mwenye nyumba hiyo, Tamara Henderson.
Hata hivyo mwanamama huyo amesema mwizi huyo alikuwa mkarimu alivyomuona mwanae. "Alimwambia mwanangu, Sahamahani, sikuwa na nia ya kukushtua, ngoja nichukue vyangu na niondoke" amesema mama huyo.

Halahala na simu

Text
Maumivu kwenye vidole gumba

Karibu nusu ya vijana wa Uingereza wanakabiliwa na maumivu ya vidole vya mikono kutokana na kutuma ujumbe katika simu za mkononi.
Utafiti uliofanywa na shirika liitwalo Fleximax umesema kijana mmoja kati ya ishirini anatuma ujumbe mwingi wa simu kwa siku hadi anapata maumivu yanayomlazimisha kuacha kufanya hivyo. Hata hivyo utafiti huo umesema, wakati vijana hao hawatumi ujumbe, wanakuwa kwenye mtandao wakirambaza huku wengine wakicheza michezo ya video.
Zaidi ya mmoja kati ya vijana kumi wanapata maumivu wakati wakitumia computer, huku asilimia 56 wanapata maumivu makali ambapo hawawezi hata kugusa miguu yao, na wengine kupatwa na maumivu ya magoti. Mkuu wa idara ya madawa Krisha Soma amesema kutokana na mabadiliko ya kimaisha, kila kizazi kuwa na changamoto yake ya kiafya.
"Na hasa ikiwa imeripotiwa kuwa vijana hutuma wastani wa text message elfu tatu kwa mwezi" amesema mtaalam huyo.Msichana mmoja amesema alianza kupata maumivu ya vidole gumba, na kulazimika kutumia dawa. "Wakati wa baridi ndio mbaya zaidi, kwa sababu maumivu ndio yanakuwa makubwa zaidi" amesema kijana huyo.

Na kwa taarifa yako.....

Kwa wastani, mtu hupiga hatua elfu kumi na nane kwa siku moja
Tukutane Wiki Ijayo... Panapo Majaaliwa...

No comments:

Post a Comment