Wednesday, November 16, 2011

Wanafunzi waliokamatwa UDSM wafikishwa kortini

Rehema Maigala na Rehema Mohamed

WANAFUNZI 50 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) waliokatwa Ijumaa wiki iliyopita wakidaiwa kujihusisha na fujo mefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali kujibu mashitaka mawili yanayowakabili.


Ilidaiwa Mahakamani hapo jana kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na kosa la  kufanya mkusanyiko usio kuwa wa halali na kusababisha uvunjifu wa amani eneo la chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Shitaka la pili ni kufanya mkusanyiko usio wa halali kwa lengo la kufanya mgomo baada ya kutolewa amri na jeshi la polisi watawanyike eneo hilo.

Kesi hiyo ilikuwa mbele ya Hakimu Bi.Waliarwande Lema, ikisomwa na Wakili wa Serikali Bw. Ladislaus Komanya, aliyeiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa wote kwa pamoja walifanya makosa hayo Novemba 11 mwaka huu eneo la Chuo Kikuu cha Mlimani.

Baadhi ya washtakiwa hao walitajwa kuwa ni Bw. Mwapamba Elias, Bw.Evalist Elias, Bw.Baraka Monasi, Bi.Hellen Moshi, Bw.Alphonce Mosako, Bi.Matrona Babu, Bi.Rolanda Willfred, Godfrey Deogratius, Bw. Moris Denis, Bi. Evonce Gumbi, Bw. Lugiko Mathias na wenzao 39.

Kati ya watuhumiwa hao 50, tisa walipata dhamana ambao ni Bi. Rehema Munuo, Bi.Grilia Masawe, Bi.Happy Amulike, Bi.Elisia Mpangala, Bi. Frida Timoth, Bi. Stella Msofe, Bw.Betwel Martin, Bw. Mmasy Stephano na Bw.Lugemalila Venance.

Watuhumiwa wengine walikosa dhamana kwa kushindwa kutimiza masharti yaliyowekwa na Mahakama hiyo ikiwemo kila mshitakiwa kutakiwa kuwa na mdhamini mmoja na bondi ya milioni moja.

Hata hivyo upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba kesi itakuja tena Novemba 28 kwa ajili ya watuhumiwa kusomewa maelezo ya awali.

No comments:

Post a Comment