Thursday, November 17, 2011
Nape ashindwa kuhudhuria kesi ya Lema
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, jana alishindwa kufika mahakamani kujibu tuhuma za kutoa kauli za kuingilia uhuru wa Mahakama, kwa kile kilichoelezwa na wakili wake, Jerome Nsemwa kwamba amelazwa katika Hospitali ya Mikocheni Mission, Dar es Salaam baada ya kuugua ghafla juzi.
Wakili Nsemwa aliimbia Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, mbele ya Jaji Aloyce Mujulizi kwamba wakati akipatwa na ugonjwa ghafla, Nnauye alikuwa tayari amekata tiketi ya ndege ambayo ingeondoka Dar es Salaam saa 12:00 jioni na kuwasili Arusha saa 1:30 usiku.
Hata hivyo, Wakali Nsemwa aliiomba Mahakama hiyo kupokea hati ya kutibiwa kwa Nnauye na tiketi aliyokata akisema atakuwa tayari kupokea maelekezo mengine ya mahakama hasa ikizingatiwa kwamba suala hilo ni la kibinadamu.
Jaji Mujulizi alikubaliana na taarifa hiyo na kuelezea kuwa shauri lililopo mbele ya mahakama ambalo linamkabili Nnuye na Mhariri wa Nipashe Jumapili, Flora Wingia ni kulinda heshima, staha na mwenendo kwa kesi kwa mujibu wa Sheria namba 114 Kifungu cha Kwanza.
Alisema kifungu hicho kinaeleza kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yoyote ambaye ataingilia mwenendo wa kesi na hukumu yake ni kifungo cha miezi sita au faini ya kiasi kisichozidi Sh500,000.
Baada ya maelezo hayo, Jaji Mujulizi alitoa nafasi kwa Wingia kuieleza Mahakama kilichotokea kutokana katika chapisho la gazeti lake na hivyo kufikia hatua ya kuitwa mahakamani hapo.
Katika gazeti hilo, Nnauye alinukuliwa akisema: “Wapo katika mkakati wa kupiga kambi kulichukua Jimbo la Arusha, wana uhakika wa kushinda kesi na kulichukua jimbo pale uchaguzi utakapofanyika.”
Wingia aliiambia Mahakama hiyo kuwa kulikuwa na upungufu wa lugha katika maandishi baada ya kupokea malalamiko juu ya kilichokuwa kimeandikwa hasa matumizi ya maneno: “Wana uhakika wa kushinda kesi.”
Aliiomba radhi Mahakama kutokana na makosa ya kiuandishi yaliyotokea na kusema wapo tayari kuomba radhi juu ya habari hiyo kwa wote walioathirika.
“Kama Mahakama itakubali, tupo tayari kuomba radhi kwa Mahakama, Mheshimiwa Godbless Lema na Nnauye katika ukurasa wa tano ilipotoka habari hii au ukurasa wa kwanza,” alisema Wingia.
Akitoa uamuzi kuhusu shauri hilo ambalo lilitokana na malalamiko ya Wakili Method Kimomogoro kuingiliwa uhuru wa Mahakama, Jaji Mujulizi alisema: “Baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa mbele yangu na Mhariri wa Gazeti la Nipashe Jumapili, nimejiridhisha kwamba maneno yaliyochapishwa yakimkariri Nnauye kuhusu uchaguzi wa Igunga ni jambo lililotokana na uzembe au kutia chumvi kwa mwandishi wa habari na uzembe na kukosa uthabiti wa Mhariri,” alisema Jaji Mujulizi.
Jaji huyo aliwaachia huru Mhariri huyo na Nnauye kutokana na madai yaliyokuwa yakiwakabili huku akiagiza gazeti hilo kuchapisha habari ya kuomba radhi kwa upotoshaji uliofanyika na kutoa onyo kwa waandishi na vyombo vya habari kuwa makini wakati wa kuandika habari zinazohusu mashauri yaliyoko mahakamani.
Mujulizi pia aliwaonya wanasiasa kuwa makini katika kauli zao zinazohusu kesi zinazoendelea mahakamani. Aliuchekesha umati uliohudhuria mahakamani hapo aliposema Nnauye alipata hofu baada ya kupata wito wa kufika mbele ya Mahakama kiasi cha kupandwa presha.
Hata hivyo, akizungumza baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Wakili Msemwa alikana kujua ugonjwa unaomsumbua mteja wake akisema uhakika alionao ni kwamba anaumwa na amelazwa.
Wingia aliondoka mahakamani hapo akiwa ndani ya gari la polisi wa upelelezi ambalo lilikuwa likisindikizwa kwa nyuma na gari jingine la polisi lililokuwa limesheheni askari wenye sare na waliovalia kiraia wakiwa wamejihami kwa silaha kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwa ajili ya usalama wao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment