Saturday, November 26, 2011

Bunge: Muswada wa Katiba unaweza kufutwa, kubadilishwa


OFISI ya Bunge imesema kuna uwezekano wa kubadilishwa au kufutwa kabisa kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, endapo itaonekana kuna sababu za msingi.Hayo yamebainishwa katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa ya Ofisi ya Bunge.

“Muswada huo, ambao Bunge liliupitishwa baada ya kuusoma kwa mara ya tatu, ambao unasubiri kuwa sheria baada ya Rais kutia saini na kuwa sheria utaendelea kusimamiwa na kutekelezwa kama sheria nyingine yoyote ambayo utekelezwaji wake unaweza kusababisha mtizamo tofauti na hivyo kupelekea kufanyiwa marekebisho endapo itaonekana kuwa ipo sababu ya kufanya hivyo na mbunge yeyote, kamati au Serikali,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:

“Kwa hiyo endapo sababu zitaonekana kuwa za msingi, basi  kubadilishwa au kufutwa wote na Bunge. Kwa hiyo kwa taratibu za uendeshaji, Bunge haikuwepo sababu ya msingi kuzuia muswada huo usisomwe kwa mara ya pili na pia hapakuwa na kanuni zozote, zilizozuia usisomwe kwa mara ya pili kwa kuwa ulikidhi mahitaji yote kikanuni.”

Ilisema baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza Bungeni, wananchi hupata fursa ya kushiriki kutunga sheria ama kwa kushiriki wao wenyewe kutoa maoni au kupitia wabunge ambao ndiyo wawakilishi wao.

“Wakati wa kujadili muswada huu mara baada ya kusomwa kwa mara ya pili na kabla haujasomwa kwa mara ya tatu, wabunge walikuwa na nafasi ya kuwasilisha mawazo yao kwa kuchangia,” ilieleza taarifa hiyo.

Imeeleza kuwa baadhi ya wabunge walitekeleza demokrasia hiyo kwa kuwasilisha mapendekezo yao pamoja na jedwali la mabadiliko.

Taarifa hiyo ya Bunge ambayo imekuja huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wakiongozwa na chama kikuu cha upinzani cha Chadema na na wanaharakati chini ya Jukwaa la Katiba, ilifafanua kuwa muswada huo ulilenga kuweka chombo ambacho kitafanya kazi ya kuchukua maoni ya wananchi ili kuyapeleka katika Bunge la Katiba ambalo litakuwa na nafasi ya uwakilishi wa kila mtu katika jamii.

Pia imesema muswada huo ni kama mingine iliyopitishwa na Bunge na unaweka utaratibu wa kuwafikia wananchi, kuwasikiliza na kupata utashi wao juu ya mapendekezo ya kuandika Katiba Mpya ili kila Mtanzania aweze kushirikishwa.

“Lakini muswada wenyewe hauhitaji ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi isipokuwa kupitia kwa wawakilishi wao; wabunge, walipitisha kwa kauli moja kuwa Sheria na siyo Katiba kama inavyoelezwa na baadhi ya wadau.”

“Bunge limeuchambua Muswada wa Sheria na kuupitisha kuwa sheria na siyo muswada wa kubadilisha katiba. Katiba sasa haitobadilishwa, bali itaandikwa upya na Serikali iliyopo madarakani kwa sasa na Bunge lake.”

No comments:

Post a Comment