RIPOTI ya Kamati Teule ya Bunge imemtia hatiani David Jairo, Katibu Mkuu aliyetolewa Wizara ya Nishati na Madini, MwanaHALISI limeelezwa.
Taarifa kutoka ndani ya serikali na Bungeni mjini Dodoma zinasema Jairo amepatikana na hatia ya kujipa mamlaka ya kutenda kinyume na maelekezo ya serikali; kukusanya fedha na kupanga matumizi yake, bila kibali cha hazina.
Mtoa taarifa wa MwanaHALISI anasema Jairo amepatikana na hatia baada ya Kamati Teule kuhoji mashahidi zaidi ya 15 wakiwamo mawaziri na watendaji serikalini.
Hata hivyo, haikuweza kusema mara moja, hatua ambazo Kamati Teule imependekeza serikali kuzichukua dhidi ya Jairo, badala yake iliwahi kuelezwa kuwa “Hawezi kurejeshwa kwenye wadhifa wake wa sasa.”
Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazomkabili Jairo, inatarajiwa kuwasilishwa bungeni mwishoni mwa mkutano wa bunge unaoendelea mjini Dodoma.
Taarifa zinasema wakati Kamati Teule inajiandaa kuwasilisha ripoti yake bungeni, Jairo anahaha kutaka kujinasua.
Mbunge mmoja wa zamani anasema mhimili huo wa dola unapita katika kipindi kingine kigumu, kutokana na Jairo kuonekana kukingiwa kifua na baadhi ya viongozi wandamizi ndani ya ikulu.
Sakata la Jairo liliibuliwa bungeni kwa mara ya kwanza na mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya nishati na madini.
Siku tatu baadaye, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo alitangaza kumpeleka Jairo likizo ya malipo, ili kupisha kile alichoita, “uchunguzi dhidi yake.”
Uamuzi wa Bunge wa kuunda Kamati Teule ulikuja siku moja baada ya Luhanjo kutangaza matokeo ya ripoti ya uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikimkabili Jairo, baada ya baadhi ya wabunge kuweka mkakati wa “kumuondoa Rais Jakaya Kikwete madarakani.”
Mpango wa kumuondoa Kikwete madarakani ulipangwa na baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hoja ya kutokuwa na imani na Rais, ilitarajiwa kuwasilishwa bungeni, mara baada ya serikali kuridhia kurejeshwa kazini Jairo.
Iliripotiwa kuwa wabunge waliotaka kuchukua hatua hiyo ni wale waliochoshwa na tabia ya Rais Kikwete ya kutowachukulia hatua wasaidizi wake hata pale wanapothibitika kushindwa kuwajibika.
Akizungumza mara baada ya mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka, Naibu Spika, Job Ndugai alisema, “…Haiwezekani, kama dharau inaweza kutokea ni hukohuko wanakofanya dharau hizi, si hapa ndani ya Bunge.”
Kauli ya Ndugai, mbunge wa Kongwa, ilionekana kuwaimarisha wabunge; na kwa maoni ya wengi, kama Rais Kikwete asingesoma alama za nyakati na kuamua kuwatosa maswahiba zake hao wawili – Luhanjo na Jairo – basi kulikuwa na uwezekano mkubwa wa yeye kujadiliwa bungeni.
Awali Sendeka akichangia hoja hiyo alisema, “…Yaliyoelezwa jana si tu hayawezi kukidhi matarajio ya bunge hili, kwa sababu ninavyopiga yowe kwamba nimeibiwa ng'ombe 100 na baadaye wakapatikana watatu, haiondoi ukweli kwamba aliyechukua ng’ombe zangu ni mwizi.”
Mbunge huyo machachari alisema, “…kitendo kilichotokea kwa kauli ya Katibu Mkuu Kiongozi, si tu kwamba kinaingilia haki na madaraka ya bunge, bali pia kinafedhehesha na kumdhalilisha waziri mkuu.”
Sakata la Jairo, kwa wachambuzi wa mambo ya kisiasa, linafananishwa na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond, kutokana na wahusika kuwa na ukaribu na viongozi waandamizi serikalini na ikulu.
Katika kashfa ya Richmond, mawaziri watatu akiwamo aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa, walilazimika kujiuzulu, jambo ambalo limeingiza CCM katika mtafaruku mkubwa, huku baadhi ya watuhumiwa wakidai “walitolewa kafara.”
Wengine waliojiuzulu walikuwa Dk. Ibrahim Msabaha aliyekuwa waziri wa nishati na madini, na Nazir Karamagi aliyekuwa amechukua nafasi yake katika mabadiliko ya kabla ya baraza la mawaziri.
Taarifa zinasema tayari Jairo amenusa kilichomo kwenye ripoti ya Bunge ndio maana ameanzisha kampeni ya kujinasua.
Tarehe 25 Agosti mwaka huu, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliunda kamati ya watu watano kumchunguza Jairo, baada ya kusafishwa kimbinu na Luhanjo.
Pamoja na mambo mengine, Spika Makinda aliipa Kamati Teule kazi ya kuchunguza utaratibu uliotumiwa na Jairo wa kukusanya fedha kutoka taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa ajili ya alichokiita Jairo mwenyewe, “ufanikishaji wa bajeti.”
Kazi nyingine ni kuchunguza iwapo utaratibu huo wa kukusanya fedha ulikuwa halali na unatambuliwa na serikali.
Aidha, Kamati Teule ilichunguza iwapo hatua ya Luhanjo, kutangaza matokeo ya uchunguzi dhidi ya Jairo, uliingilia haki na madaraka ya Bunge.
Kiongozi mmoja mwandamizi serikalini anasema, “Ni kweli hicho unachonieleza, kwamba Jairo yuko matatani. Ripoti ya Bunge imemkangaa, naye sasa anahaha kutaka kujinasua.”
Kiongozi huyo ambaye ni miongoni mwa waliohojiwa na Kamati Teule amesema, “ Kwa jinsi wale vijana walivyokuwa makini katika kufuatilia suala hili, ningeshangaa kama Jairo angetoka salama. Walikuwa wanafuatilia kila kitu.”
Kwa mfano, anasema wajumbe wa Kamati Teule walikuwa wanauliza, iwapo “utaratibu huu wa kukusanya fedha za umma uliokuwa unafanywa na Jairo, ulitumiwa na wizara yangu.
Anasema Kamati ilitaka ufafanuzi kutoka kwake, iwapo kwa uzoefu wake serikalini, amewahi kuona kitu kama hicho? Anasema, “Wamenionyesha hata barua iliyotoka Hazina kwenda kwa makatibu wakuu ikikataza utaratibu wa namna hiyo.”
Anasema, “Nami nikawaambia kwa hakika, “Binafsi sijawahi kuona utaratibu kama huo na kwamba kwangu mimi ndiyo kwanza nimeuona kwake.”
Wajumbe wa Kamati Teule iliyomchunguza Jairo, ni mbunge wa Tunduru Kaskazini, Injinia Ramo Makani (CCM), Gosbert Blandes (Mbunge wa Karagwe, CCM), Mchungaji Israel Natse (Karatu, CHADEMA), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando, CUF) na Martha Umbulla (Viti Maalum, CCM).
Katika kutafuta ukweli wa tuhuma zinazomkabili Jairo, habari zinasema Kamati ilihoji watu mbalimbali wakiwamo baadhi ya mawaziri.
Taarifa inasema Kamati ilipitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikulu na wizara ya nishati na madini, zilizoonyesha Jairo alivyokusanya mamilioni ya shilingi katika kipindi kifupi cha miezi mitatu kuelekea bajeti kuu ya taifa.
Alikusanya fedha hizo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
“Tumewahoji watu mbalimbali wakiwamo mawaziri waandamizi ndani ya serikali. Katika wote tuliowahoji, hakuna hata mmoja aliyekubaliana na utaratibu uliofanywa na ndugu Jairo,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya Kamati Teule.
Katika kuandaa ripoti yake, Kamati ya Bunge imejikita kwenye maelezo ya Jairo mwenyewe, pamoja na barua kadhaa alizoandika ikiwamo ile ya tarehe 23, 24 na 26 Juni mwaka huu, alimoagiza na kukusanya kiasi cha Sh. 85 milioni.
Barua ya Jairo iliyobeba kichwa cha maneno, “Maandalizi ya semina kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” iliagiza fedha hizo kukusanywa ndani ya siku moja.
Alisema, “…Napenda kuwafahamisha kwamba ushiriki wa wizara pamoja na kukodisha ukumbi utahitaji Sh. 39 milioni na ushiriki wa wabunge utahitaji Sh. 46 milioni.
“Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa wizara, tunashauri EWURA, TPDC, REA na TANESCO wagharamie gharama za semina ya wabunge kwa kuchangia Sh. 22 milioni kila mmoja,” alieleza.
Malipo yote alielekeza yafanywe mara moja kupitia Mhasibu wa Wizara, Bi. Hawa Ramadhani.
Vyanzo vyetu vya habari vinasema, sakata la Jairo linamuweka Luhanjo katika wakati mgumu, iwapo hasa kama Bunge litampata na hatia kama inavyoelezwa na baadhi ya walioiona ripoti hiyo.
Sababu ni mbili: Kwanza, Luhanjo ndiye aliyesimama kidete kumtetea Jairo akisema alichokifanya kilikuwa kitu sahihi.
Pili, inadaiwa ni Luhanjo anayeshinikiza kumrithisha Jairo madaraka ya ukatibu mkuu kiongozi. Kabla ya kuteuliwa katibu mkuu wizara, Jairo alikuwa katibu wa rais – Ikulu.
No comments:
Post a Comment