Saturday, November 26, 2011

Tunahitaji Mamlaka ya Gesi na Mafuta – Zitto

Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini
Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini

Haya ni maoni ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kuhusu sekta ya gesi na mafuta. Ili kujua zaidi mawazo yake, endelea kusoma makala haya.
MKUTANO wa tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mambo mengine ulijadili taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, kuhusu sekta ndogo ya gesi nchini.
Taarifa hii ilitokana na kazi iliyofanywa na kamati ndogo iliyoundwa na Kamati ya Nishati na Madini, chini ya uongozi wa Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba.
Miongoni mwa hadidu rejea za kamati ndogo zilikuwa ni kubainisha kama mikataba, taratibu na kanuni zinazotawala shughuli za gesi zinazingatia maslahi ya taifa na hazitiliwi shaka na wadau na kubainisha kama uamuzi unaoendesha shughuli za gesi kama vile gharama za ujenzi, uendeshaji na mambo mengine yanayoweza kuathiri gharama na usalama wa shughuli yanafikiwa kwa ufanisi na yanazingatia maslahi ya taifa.
Taarifa ya kamati iliwasilishwa bungeni na kupitishwa na Bunge ili Serikali iweze kutekeleza maazimio zaidi ya 26 yaliyopendekezwa.
Miongoni mwa maazimio hayo ni azimio namba mbili ambalo linasema; “Kamati imejiridhisha bila shaka kwamba  kwa kipindi cha 2004 hadi 2009 Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) imejirudishia isivyo halali gharama zinazofikia jumla ya dola za Marekani milioni 28.1 sawa na fedha za Tanzania Sh. bilioni 46.3.
“Kutokana na kujirudishia fedha hizo isivyo halali kumefanya Serikali kukosa gawio lake linalofikia dola za Marekani milioni 20.1.  Aidha, mpaka wakati Kamati inaandaa ripoti hii, Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) imeshindwa kuwasilisha uthibitisho wa uhalali wa kujirudishia gharama nyingine zinazofikia dola za Marekani milioni 36.
Hali hii inaonyesha mashaka makubwa katika uendeshaji wa sekta hii muhimu ya gesi.
Azimio hili ni moja ya maazimio yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa tunapojadili namna Tanzania inavyosimamia na kufaidika na sekta ya mafuta na gesi.
Taifa linafaidika kwa kiwango gani na wawekezaji wanafaidika kwa kiwango gani ndio msingi wa mikataba ya mafuta na gesi nchini. Bado hakuna mijadala mikali katika eneo hili ukilinganisha na mijadala katika sekta ya madini kwa mfano. Kukosekana kwa mijadala hiyo kunaachia kila kukicha Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC), kusaini mikataba ya kutafuta na kuchimba mafuta na gesi (Production Sharing Agreements – PSAs) bila Watanzania kujua haswa ni jambo gani linasainiwa. Hivi sasa kuna mikataba hii 23 hapa nchini.
Duniani kote kuna familia mbili za mikataba ya mafuta na gesi. Familia ya kwanza inaitwa ‘concessionery’ ambapo kampuni binafsi ya mafuta inapewa haki zote za mchakato mzima wa kutafuta, kuchimba, kusafirisha na kuuza mafuta au gesi.
Umiliki wa mafuta (rights) unakuwa ni wa kampuni binafsi na si Serikali. Katika mfumo huu kampuni hulipa mrabaha serikalini na kodi zinazopaswa. Nchi kama Marekani, Uingereza na Canada hutumia mfumo huu.
Familia ya pili ni mikataba ya uzalishaji au kwa Kiingereza Production Sharing Agreements (PSAs). Katika mfumo huu haki (right) inabaki kuwa mali ya taifa husika na kampuni ya mafuta huwa ni kama mkandarasi tu wa kutafuta na kuchimba mafuta. Akipata mafuta, anaondoa gharama za kuzalisha na faida inagawiwa kati ya kampuni hiyo na nchi husika kupitia Shirika la Mafuta.
Huu ndiyo mfumo unaotumika Tanzania na ulianzia huko Indonesia na Venezuela miaka ya sitini. Kutokana na mfumo huu ndiyo tunapata masuala haya ambayo Kamati ya Nishati na Madini imegundua kama nitakavyofafanua kwa ufupi hapa chini.
Mkataba wowote wa mafuta na gesi ni lazima uzingatie uzalishaji na mapato kwa ujumla, mrabaha kwa nchi, urejeshaji wa gharama za uzalishaji na kodi mbalimbali na namna faida inavyogawanywa.
Kampuni ya Pan Africa Energy kujirejeshea gharama isizostahili za zaidi ya Sh. bilioni 46 ni sehemu ya mianya iliyopo katika mikataba yetu. Jumla ya shilingi bilioni 110 zimeonekana kuwa na mashaka makubwa katika hesabu ya kampuni hii.
 
Taarifa inaonyesha kwamba kampuni hii imeweka pia gharama zao za uzalishaji kwa miradi ya nje ya Tanzania. Kwa kuwa Kampuni ya Pan Africa Energy Tanzania Limited ni kampuni tanzu ya Pan Africa Energy iliyosajiliwa ‘offshore’ Mauritius ambayo nayo ni kampuni tanzu ya Orca ambayo pia imesajiliwa visiwa vya Jersey, Tanzania isingekwepa kubambikiwa gharama ambazo si zake ili kupunguza mapato ya Serikali yake.
Imewahi kuelezwa huko nyuma kwamba hizi njia za kukwepa kodi zimeshamiri sana kutokana na kampuni kubwa zinazofanya biashara hapa nchini kufanya ‘tax planning’ na hivyo kuhamisha mapato yao kwenda nchi zisizo na kodi kubwa kama Mauritius, Isle of Man, Jersey au hata Jiji la London.
Aprili, mwaka 2009 katika taarifa yake ya mwaka, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma ililieleza Bunge kwamba mkataba kati ya TPDC na Pan Africa Energy ni moja ya mikataba mibovu kuliko yote nchini.
Hii ilitokana na ukweli kwamba kwa mujibu wa PSA kati ya TPDC na Pan Africa Tanzania, mrabaha wa mafuta wa asilimia 12 unalipwa na TPDC na pia kodi ya mapato inakokotolewa kutoka katika mrabaha huo. Kwa maana hiyo, kampuni hii hailipi mrabaha na pia hailipi kodi ya kampuni (corporate tax) kwa mujibu wa mkataba.
Suala hili Kamati ya Nishati na Madini haikuliangalia (labda kwa kuwa ni la kihesabu). Kamati ya POAC ilitaka mikataba yote ya mafuta iangaliwe upya ili kuondoa mazonge haya yanayokosesha taifa mapato makubwa sana.
Uwezo wa TPDC kukagua hesabu za kampuni za utafutaji mafuta ni mdogo au haupo kabisa. Kama TPDC wangekuwa na uwezo huu leo Kamati ya Nishati na Madini isingekuta madudu haya katika kampuni.
Pia kama Kamati ya Nishati na Madini ingeangalia mikataba ya kampuni zote za kutafuta mafuta wangekuta madudu mengi zaidi. Kuna kampuni moja yenye kisima pale Mkuranga (mkoani Pwani), wamesema gharama za kuchimba visima vile ni dola za Marekani milioni 240 ilhali gharama halisi ni dola za Marekani milioni 60 tu. Hivyo gesi ikianza kuchimbwa itabidi warejeshe gharama zao kwanza.
Tanzania haitapata lolote mpaka gesi ile itakwisha.
Kuna haja ya kufanya marekebisho makubwa sana katika uendeshaji na usimamizi wa sekta ya Gesi Tanzania. Shirika la TPDC lirekebishwe kwa kuanzisha Mamlaka ya Mafuta na Gesi yenye uwezo na nguvu ya kusimamia uwekezaji katika sekta hii.
Vilevile kuanzishwe Shirika la Mafuta na Gesi (PetroTan – National Oil and Gas Company) ambalo litashiriki katika uwekezaji  kikamilifu na kampuni binafsi. Tusiposimamia vema sekta hii, taifa letu litaingia kwenye matatizo makubwa miaka ijayo.
Maneno ya gwiji wa uchumi, Joseph Stiglitz, ni ya kuzingatia. Anasema; “Mara zote nchi zinazoendelea zijue, wanapojadiliana na kampuni kubwa za mafuta, kampuni hizi hufikiria jambo moja tu. Jambo hilo ni kuongeza mapato yao kwa kupunguza mapato ya mataifa husika.”
Tanzania ni lazima ihakikishe kwamba inapangua mbinu zote za kampuni hizi kubwa kwa kujenga uwezo wa wananchi wake kupitia Shirika la Mafuta na Gesi, ili hatimaye kuweza kuwa na mikataba yenye kujali faida kwa nchi. Hili la Pan Africa Energy litufumbue macho.

No comments:

Post a Comment