KAMATI Kuu (CC) ya CCM, imemwagiza Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete akutane na vyama vyote vya siasa badala Chadema peke yake.
Kamati hiyo imesema ni muhimu hatua hiyo ya kuzungumzia muswada wa Katiba ikafanywa kwa umakini mkubwa kwa kuwa jambo hilo, linawagusa Watanzania wengi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana Mjini Dodoma kuwa Muswada wa Marekebisho ya Katiba ni moja ya mambo yaliyojadiliwa kwa kina katika kikao hicho cha Kamati Kuu.
Agizo la chama hicho limekuja baada ya Rais Kikwete kupokea na kukubali ombi la Chadema la kukutana naye ili kujadili suala la Katiba.
Katika kutekeleza azma hiyo ya kuonana na Rais, Chadema iliunda timu ya watu saba chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambayo imepewa kazi ya kushughulikia suala hilo.
“Chama kimempongeza mwenyekiti kwa hotuba yake nzuri kuhusu mchakato wa Katiba Mpya. Pamoja na kukubali akutane na Chadema, tumetahadharisha kuwa lazima kushirikisha na wajumbe wengine kutoka vyama vyenye uwakilishi ndani ya Bunge isiwe Chadema pekee,’’ alisema Nape.
Alisema CCM kinaamini kuwa njia ya majadiliano waliyoitumia Chadema katika kutafuta haki ni nzuri na fursa hiyo ikitumiwa vizuri, inaweza kuleta maelewano mazuri na faida kwa jamii.
Viongozi wa dini wampongeza JK
viongozi wa dini, wasomi na wanasiasa, wamepongeza hatua ya Rais Jakaya Kikwete kukubali kukutana na viongozi wa Chadema ili kusikiliza madai yao juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema uamuzi huo wa Rais umeonyesha kuwa amesoma alama za nyakati na wakamtaka atafute fursa ya kukutana na wadau wengine kupata maoni yao pia kuhusu suala hilo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema ni muhimu Rais akakutana na wadau hao kwa awamu, kwa kuwa Chadema hawawezi kuwawakilisha watu wote wanaopinga muswada huo.
“Chadema wajue wana madukuduku yao ambayo si ya watu wote, hivyo kuwe na awamu ya kukutana na Rais kwa ajili ya jambo hili,” alisema.
Alisema ni muhimu Rais akawa msikivu na akazialika taasisi zote Ikulu na kujadiliana nazo ili kupata ufumbuzi wa suala hilo lililoonekana kuwa bado ni tata.
“Suala la Katiba ni kubwa na hiyo aliyofanya Rais ni hatua moja hivyo ni bora taasisi zote zihusishwe na utafutwe muda wa kukutana naye pamoja,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alisema ni muhimu kwa wadau wote wa Katiba kupewa fursa ya mazungumzo ili muafaka upatikane kwa lengo la kuwa na Katiba bora.
Zitto alisema hatua hii ya Rais Kikwete kukubali kukutana na Chadema ni njema: “Nchi haiongozwi barabarani. Kitendo cha Chadema kuachana na maandamano na kuamua kwenda kukutana na Rais na yeye kukubali hilo, nawapongeza wote,” alisema Zitto.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Makanisa ya Pentekoste Tanzania (PCT), Dk David Mwasota amepongeza hatua ya Rais Kikwete kukubali kukutana na uongozi wa Chadema.
Dk Mwasota alisema hatua hiyo ni njema na inaonyesha mwanga bora na mwelekeo wenye kuleta matumaini mapya kwa taifa. Alisema kwa muda sasa kumekuwa na matukio yanayoonyesha ishara mbaya likiwemo la mchakato wa kuandika Katiba Mpya ambao wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi walisusia mjadala wake bungeni.
“Tunampongeza Rais Kikwete, hii ni hatua inayoashiria mwanga bora kama wa asubuhi, ni imani yetu kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda na kurejesha amani na utulivu ambao tayari kumekuwa na ishara mbaya juu yake,” alisema Dk Mwasota.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alisema hatua ya Chadema kukutana na Rais ni jambo jema na inastahili kufanywa pia kwa vyama vingine vya siasa.
Alisema Rais ni mkuu wa nchi na kiongozi wa wote hivyo Chadema kutaka kukutana naye kwa ajili ya kuwasilisha madai yao wako sahihi.Kuhusu mjadala wa Katiba alisema ni mchakato unaohusu wananchi wote na kwamba wanasiasa wana nafasi yao kama ilivyo kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment