Thursday, November 17, 2011

Vurugu za Machinga Mbeya, siri nzito zafichuka

Wamachinga kwenye vurugu Mbeya
Wamachinga kwenye vurugu Mbeya
 
Machinga watumika vita ya uongozi, Meya atajwa
Wafanyabiashara wakubwa wafadhili vurugu hizo
Kituo cha Radio Mbeya FM chatumia kuchochea
VURUGU za siku mbili mfululizo za wafanyabiashara wadogo, maarufu kama machinga, Mbeya zimeibua siri nzito iliyofichika nyuma yake.
Huku wengi wakiamini vurugu hizo kusababishwa na hatua ya uongozi wa Jiji la Mbeya kuwaondoa wafanyabiashara hao kwenye maeneo yao kwa nguvu, taarifa za  ndani ya uongozi huo zinabainisha sababu kuwa ni mvutano uliopo kati ya kundi la Meya wa Jiji hilo, Athanas Kapunga, na watendaji wakiongozwa na Mkurugenzi wake, Juma Iddi.
Mvutano huo unaelezwa kuibuka tangu kuundwa kwa Baraza la Madiwani la jiji hilo, mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambapo baraza hilo lililo chini ya uenyekiti wa Meya Kapunga, liliukataa mpango uliokuwa umewasilishwa na wataalamu ukilenga kuondoa tatizo la machinga jijini humo.
Mpango huo uliowasilishwa mwishoni mwa mwaka jana na kukataliwa na wanasiasa ulitoa muda wa kuendesha biashara eneo la barabara inayoingia Kituo cha Afya cha Mwanjelwa hadi Makunguru, ambapo mpango huo uliruhusu biashara kwenye barabara hiyo kuanzia saa tisa alasiri muda ambao baadhi ya shughuli kama vile hospitali, shule na ujenzi zinapungua na watu kurejea majumbani.
Taarifa kutoka ndani ya jiji hilo zinaeleza zaidi kuwa, wafanyabiashara hao waliandaliwa eneo la barabara ya Bulongwa iliyopo hapo hapo Mwanjelwa, ambako wangendesha shughuli zao kuanzia asubuhi, na kwamba mpango huo uliafikiwa na wafanyabiashara wadogo wenyewe.
Mkurugenzi wa jiji hilo, Juma Iddi, anathibitisha hilo katika mahojiano yake na Raia Mwema, ambapo anasema kwamba wakati vurugu hizo zinatokea hakukuwa na wafanyabiashara ndogo ndogo eneo la barabara hiyo ya Hospitali ya Mwanjelwa na kwamba muda wote tangu Oktoba 28, mwaka huu, lilikuwa chini ya ulinzi sawa na maeneo mengine walikoondolewa.
Anasema uongozi uliwapangia eneo la Uhai Soweto ambalo hata hivyo, waliuomba uongozi uwabadilishie kwa madai kwamba halifai kibiashara ombi ambalo lilikubaliwa na uongozi wa jiji.
“Kamati ya Afya jana (10/11/2011) ilienda kukagua eneo waliloomba na wataalamu waliridhika, barabara ya Bulongwa ingefaa, haina msongamano, wakati timu inanipa taarifa jana asubuhi nikapatiwa taarifa askari wetu kuvamiwa, wamepigwa na gari limeharibiwa,” anasema Iddi na kuongeza,

“Nilimwita kiongozi wa machinga kumuliza akasema wao hawahusiki, alidai ni wafanyabiashara wakubwa ambao hupanga bidhaa barabarani ndio wahusika, wameshawishi vijana na wengine wametoka Mbalizi na Tunduma.”

Uhusika wa wafanyabiashara hao wakubwa pale Mwanjelwa unathibitishwa na baadhi ya wakazi wa jiji hilo wakidai kuwa wafanyabiashara hao wakubwa wa Mwanjelwa huwatumia machinga kuuza bidhaa zao kwa kupanga kwenye barabara, ikiwemo ile ya hospitali na zile za pembeni (service road) zinazopita eneo hilo la Mwanjelwa.
Vurugu za machinga hao wa Mwanjelwa zilianza saa mbili na nusu asubuhi na hadi zinaanza hakukuwa na duka lililofunguliwa, hususani yale ya upande wa kaskazini  mwa barabara hiyo, huku wamiliki wake wakiwa wamesimama nje ya maduka yao, kitendo kilichochukuliwa na wengi kuwa walifahamu mapema kuwepo kwa vurugu siku  hiyo.
Pamoja na eneo hilo, wataalamu walipendekeza pia kwa uongozi wa jiji kununuliwa kwa eneo la wazi lililopo nyuma ya chuo cha wafanyakazi nchini ili litumike na  wafanyabiashara wadogo, ushauri ambao hata hivyo ulipowasilishwa na mkurugenzi wa jiji kwenye Kamati ya Fedha ulikataliwa pamoja na mkurugenzi huyo kutenga fedha za kulinunua eneo hilo.
“Kamati ya fedha ikiongozwa na meya ilikataa kupitisha ombi la fedha lililowasilishwa na mkurugenzi kununua eneo la nyuma ya OTTU kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo,” anasema diwani mmoja kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Uchunguzi wa Raia Mwema kuhusu vurugu hizo unaibainisha hatua ya Meya wa Jiji hilo kuweka vikwazo katika mipango ya utatuzi wa suala la machinga kwenye eneo hilo la Mwanjelwa na Makunguru kugubikwa zaidi na maslahi ya kisiasa na kiuchumi.
Baadhi ya watendaji wa jiji hilo waliambia Raia Mwema kwamba Meya wa Jiji hilo ndiye mwenye kukuza mgogoro huo kwa kuweka vikwazo kwenye mipango yenye lengo la kuboresha mazingira ya kibiashara ya wafanyabiashara hao, akidaiwa kusema kwamba hatua hizo zitampa umaarufu zaidi Mbunge wa Jimbo hilo, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Sugu ambaye anatoka CHADEMA.
“Meya ndiye chanzo kikubwa sana, aliapa hawa machinga kwa sababu walichangia ushindi wa Sugu, atawaadhibu, anatumia halmashauri kutimua wamachinga, hatumii Full Council kufanya maamuzi, anatumia zaidi Kamati ya Fedha ambayo imejaa madiwani wa CCM kuendesha shughuli za halmashauri,” anasema diwani mmoja kutoka CHADEMA na anaendelea;

“Wataalamu wakipendekeza mipango ya kuondoa tatizo la machinga wanasiasa wanapinga, mkurugenzi amekuwa akitimiza majukumu yake vizuri, lakini CCM hawakubaliani naye, kwa sababu wanaona sifa zitamwendea mbunge, imefikia hatua wanamtuhumu kuwa ni chadema.”
Hata hivyo, hatua hiyo imemjenga mbunge huyo pamoja  na chama chake tofauti na matarajio ya wanamkakati hao wa CCM na ni kutokana na kauli za kigogo huyo wa CCM ambapo wamachinga hao walipotoa sharti la kutomsikiliza kiongozi yeyote zaidi ya mbunge wao.
Lakini katika hatua iliyowashitua zaidi ni pale meya huyo  huyo anapodaiwa kukaa na machinga kisha akawaelekeza kuendelea na biashara zao kwenye barabara hiyo huku akifahamu anachokisimamia kwenye mipango ya jiji hilo, ni hatua inayoibua mashaka zaidi dhidi yake.
“Tatizo hapa ni mkurugenzi, hataki sisi tufanye biashara, tulikutana na Meya alitwambia tuendele kufanya biashara, kwani wanatuandalia sehemu inayofaa, tutahamia wakitengeneza miundombinu,” anasema kijana mmoja aliyejitambulisha kuwa mmoja wa viongozi wa wamachinga eneo hilo la Mwanjelwa.
Katika mahojiano ya simu, Meya Kapunga alikiri kukutana na machinga hao akiwa na madiwani wa kata za Manga na Luanda na kukanusha madai kwamba yeye ni kikwazo uamuzi wa kuwatengea machinga maeneo yanayofaa kwa biashara zao.
“Nimeshughulikia suala la machinga pamoja na diwani wa Manga na Luanda, walitakiwa kuondoka kwenye barabara ya Hospitali ya Mwanjelwa, waliomba watafutiwe eneo, tuliwachagulia Uhai, wakasema sio pazuri, wakasema wanataka ile barabara ya Bulongwa,” anasema Kapunga na kuongeza;

“Kwa jina la Mwenyezi Mungu mi naogopa, Mkurugenzi leo alikuwa anawasilisha kwenye management, ndio limetokea, labda wameona wanachelewa.”

Kauli ya DC kuhusu uhusika wa Meya
 
Akizungumzia uhusika wa meya huyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Evans Balama, alisema si sahihi kumlaumu mkurugenzi kwa sababu hutekeleza sheria zilizotungwa na madiwani na anabainisha kuwa tatizo akisema ni madiwani ambao huwa hawawaelezi wananchi ukweli wa kile walichokiamua.
“Baraza la madiwani linaagiza watendaji, Mkurugenzi anatekeleza sheria zilizotungwa na madiwani, madiwani ni wanasiasa, hawawaelezi ukweli wananchi wao kuhusu walichoamua,” anasema Balama kisha anazungumzia madai ya ushiriki wa Meya akisema;

“Tukithibitisha hilo tunampeleka kwenye Kamati ya Maadili, actually tukithibitisha ame instigate vurugu tunamfungulia mashitaka.”

Wakati mazingira kuelekea vurugu hizo yakibainisha chanzo kuwa ni maslahi ya kisiasa, wananchi wameaminishwa chanzo kuwa ni Mkuu wa Mkoa huo, Abbas Kandoro, huku wanaosimamia hoja hiyo wakitumia zaidi historia na kudai kwamba, kiongozi huyo hapatani na machinga kutokana na sera yake ya usafi wa miji.
Hata hivyo, mpango wa kuwaondoa machinga wanaopanga bidhaa zao kwenye barabara za jiji hilo ulianza tangu uongozi wa aliyekuwa Mkurugenzi, Elizabeth Munuo, ambaye inadawi aliundiwa mizengwe na kuondolewa mara baada ya kuanza utekeleza mpango huo uliolenga kuondoa vibanda vilivyojengwa kwenye barabara za pembeni pamoja na magereji.
Baada ya mkurugenzi huyo kuondolewa, mpango wa usafishaji jiji hilo ulisimama pamoja na wataalamu kuwasilisha mapendekezo, lakini ulianza tena kutekelezwa mara baada ya kuwasili kwa Iddi kama mkurugenzi wa jiji hilo, ambapo ulienda pamoja na mpango wa udhibiti wa mapato na matumizi ya jiji hilo.
Utekelezaji wa mpango wa udhibiti wa mapato na matumizi ya jiji hilo unatajwa kuchangia kwa kiwango kikubwa mgogoro wa kiuongozi ndani ya jiji hilo kiasi cha upande ulionufaika na mapato ya jiji huko nyuma, unaongozwa na kigogo mmojawapo jijini hapo, kudaiwa kuandaa fitina za kumng’oa mkurugenzi aliyepo.
Taarifa za ndani ya uongozi wa jiji hilo na mkoani zinabainisha kuwa kundi hilo linamuona Kandoro kuwa kikwazo kwao kutokana na kauli yake ya hivi karibuni akimtaka mkurugenzi huyo kuendelea na kasi yake ya udhibiti wa mapato ya jiji hilo na kwamba, atamlinda huku akitangaza vita dhidi ya wale wenye kuandaa njama za kuwang’oa wakurugenzi kwa maslahi yao.
Radio ya Jiji Mbeya yachochea vurugu

Baadhi ya wakazi jijini humo, wakiwamo wanahabari wamefikia hatua ya kuhoji ajenda nyuma ya kituo cha redio inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, kurusha vipindi vilivyochochea zaidi vurugu hizo na kujenga chuki dhidi ya baadhi ya viongozi, hususani mkuu huyo wa mkoa.
Kituo hicho kilirusha matangazo ya moja kwa moja huku ajenda ikiwa utendaji wa mkuu wa mkoa. Ni hatua hiyo inayoelezwa na wafuatiliaji wa vurugu hizo iliyojenga mtazamo hasi kwa wananchi dhidi ya mkuu huyo wa mkoa kwamba, oparesheni hiyo iliendeshwa kwa maagizo yake, wakati ikifahamika ya kuwa kiongozi huyo ndio kwanza akianza ziara ngazi ya wilaya na taasisi mbalimbali mkoani humo kujitambulisha.
Utendaji wa kituo hicho, ikiwamo matumizi ya matusi, kashfa, ukithibitisha nguvu isiyo na mipaka ya vyombo vya habari iwapo vitatumika vibaya, umelalamikiwa hata na wanahabari wenyewe wakati wa mkutano wa waandishi wa habari na Kandoro, uliohudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Kamanda wa Polisi Mkoa, Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa na Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya.
Mkurugenzi wa jiji hilo alikiri kupokea malalamiko kuhusu uchochezi unaofanywa na kituo chake na kwamba tayari wameanza kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji huo wa maadili.
Polisi lawamani kuchochea mapigano

Matumizi ya nguvu kupindukia kutuliza vurugu hizo imetajwa pia kwamba ndiyo iliyochochea kuwepo kwa mapambano makali kati ya wananchi na askari wa Jeshi la Polisi, ambapo yalitumika mabomu ya machozi na risasi za moto zilizosababisha mauaji ya wananchi wawili na majeruhi watano.
“Vurugu zilianzishwa na kikundi kidogo sana, hawakuzidi vijana 50, yale mabomu ya machozi ndiyo yaliyoamsha hasira za wananchi, kila walipolipua ndivyo watu walipozidi kuja Mwanjelwa na kujiunga kwenye mapambano na polisi,” anasema mkazi mmoja wa Mwanjelwa.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Malindisa alidai kuwa nguvu iliyotumika haikuwa kubwa bali walitumia ile ya busara.
“Ni tafsiri tu, nguvu inayotumika sasa ni ya busara, ni reasonable force, hakuna nguvu yoyote ya ziada kwa maana ya excessive force iliyotumika,” anasema Malindisa.
Mbali ya matumizi ya nguvu kubwa, jeshi hilo linalaumiwa kwa kuwashambulia watu wasiohusika na vurugu hizo ambapo walirusha mabomu kwenye majengo yaliyoko pembezoni mwa barabara huku wakiwaacha vijana waliokuwa wakipambana nao ambao walitamda barabarani.
Kukosekana kwa umakini miongoni mwa askari polisi walioshiriki zoezi hilo kulisababisha polisi hao kuua na kujeruhi raia wasiohusika waliokuwa mbali, zaidi ya mita 300 kutoka eneo la tukio ambako walikuwa wakiendelea na shughuli zao.
Taarifa iliyowasilishwa kwa mkuu wa mkoa iliwaelezea kuwa walikutwa wakitaka kupora Benki ya Barclays, jambo linalokosa ukweli kutokana na benki hiyo kudaiwa kuvamiwa nyakati za jioni wakati waliouawa na kujeruhiwa ilikuwa ni nyakati za mchana.
Sugu azungumza na wafuasi wake
Ilichukua takribani nusu saa kwa Mbunge wa Mbeya, Joseph Mbilinyi, kuwasihi wafuasi wake wanaodaiwa kuhusika katika mgogoro huo. Alifanikiwa kuwatuliza kwa kuwapa pole na kuwasihi kuendelea na shughuli zao. Hata hivyo aliwageukia viongozi hususani wa chama tawala akiwaeleza wabadilike.
“Kimsingi machinga mna madai ya haki yaliyosababisha mliyoyafanya jana, tukio la jana liwe somo kwetu sote kwamba huu sio wakati wa kuendesha mambo kisiasa, ni wakati wa kufanya mambo kisayansi,” alisema mbunge huyo katika mkutano wake na wananchi uliofanyika kwenye kituo cha mabasi cha Kabwe uliohudhuriwa na umati mkubwa.
Wafanyabiashara hao walitoa sharti la kutomsikiliza kiongozi yeyote zaidi ya mbunge wao kutokana na msimamo unaodaiwa kuwekwa na meya wa jiji hilo, wa kuwashughulikia wafanyabiashara hao kwa kitendo chao cha kumchagua Mbilinyi.
Taarifa za ndani ya kikao cha uongozi wa mkoa na jiji zinaeleza kuwa mvutano ulijitokeza kuhusu mbunge huyo kukutana na wamachinga kwa baadhi ya viongozi kupinga, na ndipo mkuu wa mkoa huo alipoingilia kati kwa kuagiza kwamba mbunge achwe akazungumze na wapiga kura wake.
Mvutano kama huo ulijitokeza pia siku ya kwanza ya vurugu hizo, ambapo inaelezwa kuwa mkuu wa wilaya alibaini mapema kushindwa kwa jeshi la polisi kudhibiti vurugu hizo hivyo kushauri kuomba msaada wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lakini uongozi wa jeshi la polisi mkoani humo ukagoma kukiri kuelemewa.
Wakati wa kampeni za ubunge wa jimbo hilo mwaka jana, CCM ilipata wakati mgumu eneo hilo la Mwanjelwa ambapo vijana walikiunga mkono CHADEMA wazi wazi hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa ushindi wa Mbilinyi.
Vurugu za Mwanjelwa zimesababisha  madhara makubwa jijini Mbeya ikiwemo kifo cha kijana mmoja mwendesha pikipiki huko Uyole aliyeuawa na polisi, watu watano waliojeruhiwa kwa risasi za polisi na wengine zaidi ya 300 kushikiliwa na jeshi hilo.
Kwa mujibu wa Kandoro, hadi Jumapili wiki hii watuhumiwa wote walikuwa wameachiwa huru isipokuwa 35 tu waliofikishwa mahakamani Jumatatu wiki hii, na kuachiwa baada ya kujidhamini wenyewe.
Kutokana na Jeshi la Polisi kuzidiwa nguvu na wananchi, Serikali ya Mkoa iliomba msaada wa Jeshi la Wananchi ambao kwa kuwatumia vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walituliza vurugu hizo bila matumizi yoyote ya nguvu kubwa.

No comments:

Post a Comment