Saturday, November 19, 2011

Ukoo wa CHADEMA bungeni waanikwa

 BAADHI ya wabunge wameiumbua CHADEMA, wakieleza kuwa chama hicho ndicho kinaongozwa kwa utawala wa kifalme.bAkichangia juzi, muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011, Assumpter Mshama (Nkenge – CCM), alisema utawala wa kifalme upo CHADEMA.b“Mfadhili wao amekuja na mtoto wake, kuna mdogo wake, ukienda kwa Lissu kaja na dada yake. Ukienda kwa mwenyekiti wa chama ana ndugu watatu, nani ameleta ufalme zaidi,” alihoji.bAliongeza: “Slaa kuna mke wake, nani ana utawala wa kifalme, Ndesamburo amekuja na mtoto wake na mkwe wake, samahani mheshimiwa Ndesamburo.
“CCM ilitengeneza utaratibu wa kupata viongozi wa viti maalumu, wao si kifalme tu, tuseme ni Kaskazini tu, nawashangaa watu wanaojiita CHADEMA, wenzako wako bungeni huulizi wamepatikanaje.”bKwa upande wake, Livingstone Lusinde (Mtera - CCM), akichangia jana, alisema CHADEMA ndiyo yenye tabia ya kupeana madaraka kwa kufuata unasaba.
Alisema viti maalumu vimetolewa kwa unasaba, na kama hilo lingefanywa na CCM ingekuwa wimbo kila siku.
“Ndiyo maana humu ndani wamo wakwe, dada, kaka, ingekuwa ni kwa CCM ingekuwa wimbo kila siku. Nashangaa wanaposema rais anaongoza kifalme,” alisema. Ingawa Lusinde hakuwataka kwa majina ndugu hao wa viongozi wa juu wa CHADEMA, lakini inafahamika kwamba, Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, mtoto wake ni Lucy Owenya na mkwewe ni Grace Kiwelu ambao ni wabunge wa viti maalumu.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbrod Slaa mkewe Rose Kamili naye ni mbunge wa viti maalumu, kama kwamba haitoshi Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu naye ana dada yake, Christina Mughwai ambaye ni mbunge wa viti maalumu.
Kigogo mwingine wa CHADEMA, ambaye ni Makamu Mwenyekiti Zanzibar, naye ana mtoto wa dada yake bungeni kupitia nafasi hizo. Mjomba wake kigogo huyo ni Raya Ibrahim Khamis.

Lusinde alisema wanaotoa vitisho vya kuandamana na kwamba wapo tayari kufa kwa ajili ya katiba waachwe wafanye hivyo, kwani wa kuzuia fujo wapo.
 
“Wanaotaka kufanya vurugu waachwe tu, wengine wanasema wapo tayari kufa kwa ajili ya katiba. Mimi sipo tayari nataka nione katiba mpya, ambayo Watanzania wamekuwa wakiitaka kwa muda mrefu,” alisema.
Lusinde alihoji busara ya wazee wa CHADEMA ambao wameshindwa kutoa kauli baada ya vijana wao kuchafua hali ya hewa.
Mbunge huyo alisema CHADEMA inafanya hivyo kutokana na ahadi ya fedha waliyopewa na Ujerumani.
CHADEMA imesusa kujadili muswada huo unaohitimishwa leo, baada ya kujadiliwa kwa siku nne, kwa kile wanachodai umekosa uhalali kwa kukiuka Kanuni za Bunge.
Hata hivyo, CHADEMA imekuwa ikijibu hoja zinazojadiliwa na wabunge bungeni, kupitia mikutano na waandishi wa habari inayofanyika kila siku mchana, ambapo katika mkutano wa jana imeliomba bunge kutopitisha muswada huo.
Mikutano hiyo imekuwa ikiitishwa na viongozi wa CHADEMA, John Mnyika (Ubungo) na Tundu Lissu (Singida Mashariki), ambaye Jumatatu wiki hii aliwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni, kuhusu muswada huo.
Katika maoni hayo, alipendekeza baadhi ya mambo kwenye muswada huo ambayo yaliwachefua wabunge kutokana na hoja zake kuhusu Muungano, na pia kutamka kuwa Tanzania ina urais wa kifalme.
John Lwanji (Manyoni Magharibi - CCM), alisema wanachofanya CHADEMA ni sawa na kiini macho katika mazingaombwe, akitumia neno 'abrakadabra'.
Benardetha Mushashu (Viti Maalumu - CCM), alihoji CHADEMA walitoka bungeni kwa kanuni gani na mbona hawachukuliwi hatua.
“Wanawalaghai wananchi, Lissu alichangia muswada. Wanaharakati wanatangaza kufanya maandamano yasiyo na kikomo kana kwamba hakuna serikali, wakijaribu wataona,” alisema.
Alisema kinachoendelea Arusha ni matokeo ya maandamano ya kila siku, ambayo hivi sasa yameanza kushamiri Mwanza, ambapo watu wanapigwa mabomu ya machozi.
“Libya walianza na maandamano, Gaddafi ameuawa, lakini hivi sasa wanauana,” alisema.
Wakati huo huo, Spika  wa Bunge, Anne Makinda, amesema hamlazimishi mbunge kuingia kwenye kamati, bali anachofanya ni kufuata Kanuni za Bunge na Katiba.
Alisema hayo bungeni jana, kutokana na malalamiko yanayotolewa na CHADEMA na NCCR-Mageuzi kwamba, spika alilazimisha wabunge kuingia katika Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, kujadili muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.
Spika Anne alisema CHADEMA hawakutumia busara kutoka ndani ya ukumbi wa bunge, bali wangewasilisha hoja zao, na endapo wangeshindwa, basi wangeshindwa kishujaa.

No comments:

Post a Comment