Thursday, November 24, 2011


Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen ametia saini makubaliano ya kujiuzulu kwake.
Bw.Saleh alitia saini makubaliano hayo yaliyopendekezwa na nchi jirani za ghuba katika mji mkuu wa Saudi Arabia , Riyadh.
Chini ya makubaliano hayo atamkabidhi madaraka naibu wake kabla ya uchaguzi mkuu utakaotishwa mapema na yeye mwenyewe atapata msamaha wa kinga ya kufikishwa mahakamani.
Lakini baadhi ya waandamanaji nchini Yemen wamesema watakataa makubaliano yoyote ambayo yatampa kinga rais na maafisa wake.
Waandamanaji hao walisema mpango huo wa nchi za Ghuba umepuuza "damu ya mashahidi."
Hatua ya serikali kupambana na waandamanaji imesbabaisha vifo vya mamia ya watu na maelfu kujeruhiwa nchini Yemen.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 69 aliyetawala tangu 1978 amekabiliwa na maandamano tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Mara kadhaa alionekana kuwa tayari kutia saini makubaliano lakini alikuwa akibadili nia yake dakika za mwisho.
Wakati huo huo kumezuka mapambano kati ya wanajeshi wanaomuunga mkono Rais Saleh na wapiganaji wa kiongozi muasi wa kikabila Sheikh Sadiq al-Ahmar katika wilaya ya al-Hasaba mjini Sanaa,ingawa taarifa za awali hazikueleza kama kulikuwa na maafa yoyote.

No comments:

Post a Comment