Saturday, November 26, 2011

Pinda, Makinda ‘wavuta’ za Jairo

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
 
Wabunge ‘wakunja’ milioni 16
Ripoti Kamati Teule ina utata

SEHEMU ya mamilioni ya fedha zilizochanganishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, zimelipwa pia kwa wabunge kupitia semina, akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baadhi ya mawaziri na Spika, Anne Makinda, Raia Mwema, imebaini.
Pinda na Makinda walikua katika kundi moja na Diana Chilolo (Mwenyekiti wa semina), John Joel (Mwakilishi wa Katibu wa Bunge) na January Makamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ambaye hata hivyo jina lake lilikatwa na hakuwa amesaini karatasi ya malipo hayo ya Shilingi 280,000 kila mmoja.
Mbali na Spika na Waziri Mkuu, wengine waliosaini fedha hizo ni mawaziri na wabunge kadhaa wa wakiwamo wale maarufu wa vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CCM, katika semina iliyofanyika Juni 26, mwaka huu, mjini Dodoma kuhusu sekta ya umeme nchini ambao wao walilipwa Sh.110,000 kila mmoja.
Miongoni mwa wabunge wakiwamo maarufu ambao hata hivyo utaratibu wa malipo kwao katika semina ni wa kawaida ni pamoja na Mchungaji Israel Natse (Karatu), Augustino Masele (Shinyanga Mjini) na Diana Chilolo (Vitimaalumu mkoani Singida).
Wengine ni Hamad Rashid Mohamed (Wawi), Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Binilith Mahenge (Makete), David Kafulila (Kigoma Kusini), Davidi Silinde (Mbozi Magharibi), Moses Machali (Kasulu Mjini), Grace Kiwelu (Vitimaalumu-Kilimanjaro), Augustino Mrema (Vunjo), Profesa David Mwakyusa, Kassim Majaliwa na Kheri ali Khamis.
Wabunge wengine kwenye orodha hiyo ni Naomi Kaihula, Maria Hewa, Cynthia Ngoye, Peter Msolla, Juma Nkamia, Esther Matiko, Joseph Selasini, Mohummad Sanya, Tundu Lissu, Stela Manyanya, Lucy Owenya, Ezekia Wenje, Cristina Mughwai, Leticia Nyerere, Livingstone Lusinde, George Simbachawene na Gosbert Blandes.
Mawaziri katika orodha hiyo ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Bunge na Uratibu, William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawan Ghasia, Naibu Waziri wa Fedha, Gregory Teu, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athumani Mfutakamba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji na Uwezeshaji, dk. Mary Nagu.
Wengine ni Naibu Waziri wa Maji, Gerson Lwenge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanry, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Milton Mahanga na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba.
Wakati malipo hayo ya posho kwa viongozi hao yakiwa hayana utata, hali imekuwa tofauti kwa watumishi wengine wa Serikali waliolipwa fedha hizo. Baadhi wakiwa wamelipwa na kusaini Sh. 20,000 tu, tarakimu hizo zimeghushiwa na wahasibu husika na kuonekana wamelipwa Sh 120,000.
Kutokana na kasoro kubainika katika mchakato wa matumizi ya fedha hizo ambazo ukusanyaji wake haukidhi vigezo vya kisheria na taratibu, Kamati Teule iliyoundwa kuchunguza sakata hilo, imependekeza sasa Bunge kujadiliana na Serikali ili hatimaye kutenga fungu maalumu kwa ajili ya semina za wabunge, badala ya sasa ambapo fedha hazikujulikani zimepatikana vipi na kisha kulipwa kwa wabunge au viongozi wengine wakiwamo mawaziri.
Kamati hiyo teule iliyoongozwa na Mbunge, Ramo Makani inaeleza katika ripoti yake; “Kamati Teule inapendekeza Bunge lijadiliane na Serikali kuhusu namna bora ya kuendesha semina kwa wabunge, ikiwamo kutenga kasma mahususi ndani ya Mfuko wa Bunge na kusisitiza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya fedha.
Utata ripoti ya Kamati Teule
Kwa upande mwingine, ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, imetoa taarifa yenye mgongano na hasa mapendekezo yake kuhusu kuwachukulia hatua Waziri William Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima.
Utata unajitokeza pale ambapo kamati hiyo licha ya kupendekeza viongozi hao wachukuliwe hatua lakini inakiri kuwa hawajabaini ushiriki wa viongozi hao katika uchotaji wa fedha hizo.
Sehemu ya ukurasa wa 144 wa taarifa hiyo inasomeka; “Katika suala la uchangishaji fedha uliofanywa na Wizara ya Nishati na Madini, kamati teule baada ya kukamilisha uchunguzi kwa kupitia nyaraka mbalimbali na kufanya mahojiano na watu mbalimbali, haikuweza kuthibitisha moja kwa moja ushiriki wa Waziri au Naibu Waziri, katika kubariki au kuidhinisha uchangishaji huo.”
Hata hivyo, kamati hiyo licha ya kukiri kushindwa kuthibitisha uhusika wa Waziri na Naibu wake, imependekeza wachukuliwe hatua kwa kujificha katika ‘kichaka’ kuwa viongozi hao walipaswa kujua kila kinachoendelea katika wizara yao.
Hali hiyo ya utata ndiyo iliyotumiwa na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, kumtetea Waziri Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima, kwamba hakuna uthibitisho wa kuhusika kwao katika uchotaji wa fedha hizo.
Wengine waliochangia katika mwelekeo huo ambao pia walionesha wazi kuwa tatizo la msingi ni mfumo na si mtu ni pamoja na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, Mbunge wa Same Mashariki na Anne Kilango Malecela.
Wabunge hao kila mmoja kwa wakati wake walipokuwa wakijadili ripoti hiyo bungeni wiki iliyopita mjini Dodoma walieleza kuwa ni wakati muafaka kwa mfumo mzima wa Serikali kubadilishwa na hasa katika eneo la matumizi ya fedha za umma.
Katika hatua nyingine imebaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini ndiyo inayoongoza kujilipa posho kubwa katika masuala ya shughuli zake za kibajeti ndani ya Bunge, ikilinganishwa na wizara nyingine.

No comments:

Post a Comment