Saturday, November 26, 2011

‘Gamba’ laendelea kuisumbua CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekiri kuwa mwito wa ‘kujivua gamba’ kwa viongozi wake wanaotuhumiwa kwa ufisadi haujaitikiwa kiasi cha kuridhisha na walengwa.

Kutokana na hali hiyo kimeagiza kamati za maadili na usalama katika ngazi zote nchi nzima kuwachukulia hatua haraka watuhumiwa wote.

Aidha, watuhumiwa wa ngazi ya kitafa nao mbali na kutakiwa kushughulikiwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya Taifa inayoundwa na viongozi wakuu wa Chama na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu, pia tuhuma zao zitachunguzwa.

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alisema hayo jana wakati akisoma maazimio ya kikao cha siku mbili cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kilichomalizika juzi na kuongeza kuwa watuhumiwa hao watachunguzwa na Kamati Ndogo ya Uchunguzi itakayosimamiwa na Makamu Mweyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa.

Mbali na Msekwa, wajumbe wengine wa Kamati hiyo itakayofanya kazi hiyo na kuwapa nafasi ya kujitetea kabla ya kuwachukulia hatua watuhumiwa hao, ni Mukama mwenyewe na wajumbe wengine wanne; wawili kutoka Zanzibar na wawili Tanzania Bara.

Mukama pia alikiri kuwapo harakati za urais wa mwaka 2015 huku akilaani viongozi wanaoacha majukumu yao ya kiserikali na kujikita katika harakati hizo.

Pia alikiri uwepo wa alichokiita saratani ya kupanga safu za viongozi katika uchaguzi na kuelezea hatua zitakazochukuliwa kukabiliana na hali hiyo.

Mukama alirejea moja ya maazimio ya NEC Aprili mwaka huu; "Kwa kutambua kuwa suala la ufisadi limekuwa mzigo mkubwa sana kwa chama licha ya juhudi kubwa ambazo Serikali imezifanya kupambana nalo, Nec ilielekeza kuwa CCM lazima ipige vita ufisadi kwa nguvu kubwa zaidi na ionekane inafanya hivyo ndani yake
yenyewe.

"Nec iliamua kuwa viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama. Wasipofanya hivyo, chama kiwawajibishe bila kuchelewa," alimaliza kunukuu azimio hilo la Nec.

Alisema azimio hilo lilikuwa sehemu ya mageuzi ya kukipa chama sura mpya maarufu ‘kujivua gamba’, lakini akafafanua kuwa utekelezaji wake baada ya miezi saba tangu litolewe, haujaridhisha.

"Hali ilivyo sasa, takribani miezi saba baada ya azimio hilo kupitishwa, bado hatujapata mwitikio wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi zote za chama chetu, ambao ni walengwa wa azimio hilo.

"Bila shaka wakati umefika kwa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika ... kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kanuni za CCM za uongozi na maadili," alisema Mukama.

Alisema, mbali na Kamati Ndogo ya Uchunguzi ambayo iko chini ya Kamati Kuu ya CCM, pia Nec iliagiza kamati za maadili na usalama nchi nzima, kuwachukulia hatua viongozi wanaotuhumiwa kwa haki na kuwapa fursa ya kujitetea na kupeleka taarifa kwa mamlaka za uteuzi za viongozi hao.

Mukama alifafanua, kuwa wako watakaochukuliwa hatua na mamlaka za wilaya, za mkoa na Taifa na hilo litatekelezwa wa kuzingatia Mamlaka iliyomteua au kumwidhinisha kiongozi husika.

Katibu Mkuu aliyefuatana na Msekwa na Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alifafanua kuwa hali ya siasa ndani ya chama hicho ni shwari, lakini si shwari sana.

Alisema chama kinakiri kuwapo harakati za viongozi wake kugombea urais mwaka 2015 na kuongeza kuwa hazina madhara kwa chama huku akinukuu kauli za kiongozi wa China, Mao Dze Dung kuwa waache mawazo na fikra 100 zishindane na fikra pevu
zitajidhihirisha, jambo lililoonesha kuwa harakati hizo zimeruhusiwa.

Hata hivyo, alionya kuwa harakati hizo zinatakiwa kufuata utaratibu, kuepuka kugawa wanachama katika makundi na kuepuka kuchafuana, kama njia ya kujitangaza, huku akilaani viongozi walioweka pembeni majukumu ya kiserikali na kujikita katika harakati za kutafuta urais.

Pia alikiri kuwapo alichokiita saratani ya kupanga safu ya viongozi huku akionesha kuwa inaweza kutokea katika uchaguzi wa ndani ya chama mwakani.

Alisema ili kuepuka harakati za urais zisilete madhara na kumaliza saratani ya kupanga safu, CCM inajipanga kuwa wazi katika uchaguzi wa ndani wa mwakani ili kipate viongozi watakaohaghaika na wavuja jasho.

Mbali na uongozi katika chama, Mukama alisema pia CCM inatafuta utaratibu mzuri wa kumpata mgombea urais usiotegemea makundi na fedha na kuongeza kuwa mgombea atapimwa kwa msimamo wake katika itikadi ya chama hicho na hoja zake za kupambana na umasikini wa Watanzania.

Kwa mujibu wa Mukama, ajenda ya mageuzi imepokewa vyema hasa na viongozi kwa kuwa kabla ya kuanzisha kwa ajenda hiyo, viongozi wa CCM walifikia mahali wakawa kama kuku kwenye tenga ambao wakifunguliwa watoke, hubakia wamezubaa.

Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa mageuzi hayo kufanyika kwa utaratibu, ili kuzuia mpasuko huku akionekana kutofautiana na falsafa ya Nape ya kuoga kwa kuanzia kichwani kwenda mwili mzima, kwa kusema kuwa watu wanaoishi kando ya ziwa, huanza kujaribu maji kwa mguu na kuingia kuanzia chini kwenda juu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martine Shigella, amekana taarifa za kuwapo mkakati wa kuasi ndani ya chama hicho, huku akikiri kuwa taarifa hizo za uasi 'zimechangia' wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kuzingatia maslahi ya chama.

Akizungumza jana muda mfupi baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kutoa taarifa ya maazimio ya kikao cha Nec kilichomalizika juzi, Shigella alisema hata taarifa za uasi hazikutolewa na kiongozi wa umoja huo na kwamba kwa kuwa jumuiya hiyo ni ya CCM haiwezi kuasi chama.

Alipotakiwa kueleza sababu za wenyeviti wa umoja huo kutoka mikoa 17 nchini na makatibu wao kupiga kambi Dodoma wakati wa kikao cha Nec, alisema hana taarifa ya ujio wa viongozi hao, wala sehemu waliyosaini ingawa gazeti hili lilishuhudia wakiletwa na mabasi yenye bendera za chama hicho.

Hata hivyo, pamoja na kukana kuwapo kwa viongozi hao, Shigella pia alikiri kuwaona baadhi na kuongeza kwamba walikuja kusikiliza yanayoendelea katika vikao hivyo kwa karibu.
Shigella pia alimpongeza Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kwa kuongoza vema vikao vya Kamati Kuu na Nec, kwa maelezo kuwa watu walichotarajia hakikutokea, lakini bila kufafanua.

No comments:

Post a Comment