Tuesday, November 22, 2011

Mwendesha ‘bodaboda’ awapora majambazi bastola

Keneth Goliama
MWENDESHA pikipiki zinazobeba abiria maarufu ‘bodaboda’ amefanikiwa kuwapora bastola majambazi wawili, ambao pia walifanikiwa kumpora pikipiki aliyokuwa akiitumia.

Katika kazi yake, mwendesha pikipiki huyo aliyejitambulisha kw ajina la Athuman Juma, alikabiliana na majambazi hao katika eneo la klabu ya Biashara, Temeke, iliyoanza mara tu alipoanza kudai malipo yake kwa mteja aliyemsafirisha kutoka kituo chake cha Vetenary, Temeke.

Akizungumza katika ofisi za Mwananchi,  Juma alisema tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa moja jioni baada ya mtu huyo kufika katika kituo hicho cha Vetenary na kumtaka ampeleke katika ukumbi huo wa klabu ya Biashara, Temeke.

Kijana huyo alisema baada ya kumfikisha eneo la klabu hiyo, alipokuwa akidai malipo yake alijitokeza mtu mwingine kutoka ndaniya ukumbi huo aliyekuwa na bastola na kumuamuru kushuka kwenye pikipiki, akitaka pia amkabidhi simu yake ya kiganjani.
Juma alisema baada ya kuona hivyo, aliamua kushuka kwenye pikipiki na kumkabidhi mteja huyo aliyekuwa amemkodi lakini  akafanikiwa kumshika kijana huyo aliyekuwa na Bastola, ndipo  walipoanza kupambana wakiing’ang’ania bastola na kusababisha risasi moja kufyatuka bila kumdhuru yeyote miongoni mwao.

Alisema baada ya purukushani hizo alifanikiwa kumnyang`anya jambazi huyo bastola, ambapo baada ya kuona wamezidiwa nguvu waliamua kukimbia na pikipiki wakitokomea kusikojulikana.

“Vurugu ilikuwa kubwa ya kunyang`anyana ile bastola, lakini niliwashinda na kuweza kuchukua bastola, ndipo wakakimbia na pikipiki maana walikuwa wameshachukua funguo,” alisema.

Alisema baada ya tukio hilo kutokea alijitokeza mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa yeye ni askari wa upelelezi jijini Dar es Salaam na kumtaka kupeleka bastola hiyo kituo cha Polisi cha Kilwa Road ili aweze kuandika maelezo.
“Hakika wakati wa tukio lile niliogopa sana kutokana na wale watu kuwa na bastola lakini baada ya kupata ujasiri nilipambana nao na kuwashinda,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kuwatafuta majambazi hao na kuwasihi wanachi kuwapa polisi ushirikiano wa kutosha.

 Misime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la ujambazi na kushukuru kijana huyo kwa ushujaa alioonyesha wa kupambana na  majambazi hao na kusihi kuwa Jeshi la Polisi litatoa zawadi kwa  wananchi wanaoshirikiana na jeshi hilo katika kuimalisha ulinzi shirikishi.

No comments:

Post a Comment