Monday, November 28, 2011

JK apokea kabrasha la Chadema


RAIS Jakaya Kikwete jana alikutana na ujumbe wa Chadema na kukabidhiwa kabrasha la mapendekezo ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini na kisha kujadili mchakato wa utungwaji wa Katiba Mpya.

Rais alikutana na viongozi hao kuanzia saa 9:30 alasiri mpaka saa 12:00 jioni. Mara baada ya ujumbe huo wa Chadema ulioongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwasili Ikulu, ulipokewa na Rais Kikwete na muda mfupi baadaye wote wakatoka nje na kupiga picha za pamoja kabla ya kurejea ndani ambako pia walipiga picha nyingine za makabidhiano ya kabrasha hilo la mapendekezo ya Chadema na hatimaye kuendelea na majadiliano.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema kwamba kikao cha jana hakikumalizika na kimeahirishwa hadi leo saa nne.

“Pande zote mbili zimekubaliana kukutana tena asubuhi ya kesho (leo), ili kuipa nafasi Serikali iweze kutafakari mapendekezo hayo,” ilisema taarifa hiyo.

Mbowe alithibitisha kwamba kikao hicho kitaendelea leo na taarifa zote zitatolewa baada ya hapo... “Ndugu waandishi wa habari tumekutana na Rais na baadhi ya mawaziri na wasaidizi wake. Kikao kilianza saa 9:30 mchana na kiliahirishwa saa 12:00 jioni. Kikao kitaendelea kesho asubuhi saa nne. Taarifa kamili ni baada ya kikao.”

Hata hivyo, taarifa ya Ikulu imesema pande hizo mbili zimekubaliana kuwa Katiba ya sasa ni nzuri iliyolilea Taifa kwa miaka 50 iliyopita na ndiyo iliyoliwezesha Taifa la Tanzania kuwa na amani, utulivu.

Mbali ya kukubaliana katika hilo, Ikulu imesema Kikwete na ujumbe huo wa Chadema wamekubaliana juu ya umuhimu wa kutunga Katiba Mpya kama Rais Kikwete alivyoliahidi taifa wakati wa salamu zake za mwaka mpya Desemba 31, mwaka jana.

“Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Rais aliwahakikishia wajumbe hao wa Chadema kuwa ni dhamira yake na ya Serikali yake kuhakikisha kuwa Tanzania inapata Katiba Mpya,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu na kuongeza:

“Katika mkutano huo, pande zote mbili zimekubaliana kuwa ni jambo muhimu kwa mchakato mzima wa kutungwa kwa Katiba Mpya kuendeshwa kwa namna ya kulinda na kudumisha tunu za taifa za amani, utulivu na umoja wa kitaifa.
Aidha, pande zote mbili zimekubaliana kuwa mchakato huo uendeshwe kwa kuzingatia misingi ya mambo mengine muhimu kwa taifa la Tanzania kama vile kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, kuligawa Taifa kwa misingi ya udini na ukabila ama kutugawa kwa misingi ya maeneo.”

Mbowe aliongozana na wajumbe wa kamati maalumu iliyoteuliwa na Chadema kwa ajili ya kuonana na Rais Kikwete ambayo wajumbe wake ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Said Arfi, Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) Said Issa Mohamed, Mshauri wa Masuala ya Siasa wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lisu, ambaye alikuwa Katibu wa Kamati hiyo. Pia alikuwapo John Mrema lakini Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa ambaye ni mjumbe hakuwepo.

Kwa upande wa Serikali, mbali ya Rais Kikwete alikuwapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi.

Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Mkutano huo umefanyika baada ya Rais Kikwete kuafiki ombi la Chadema la kutaka kuonana naye kwa lengo la kumweleza kasoro zilizopo kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ambao tayari umeshapitishwa na Bunge ukisubiri kusainiwa na Rais ili kuwa sheria.

No comments:

Post a Comment