Saturday, November 12, 2011

Sakata la Zitto kudaiwa kutaka Uenyekiti wa Mbatia NCCR Mageuzi

.Yeye amjia juu Kafulila akitibwa India
.Asema hatakihama Chadema amekitumikia kutoka utotoni
.Asema vijana wasiwe waongo kama wazazi wao

Peter Mwenda na Flora Amon
MGOGORO wa Chama cha NCCR Mageuzi umechukua sura mpya, baada ya kuibuliwa madai kuwa njama za kutaka kumng'oa mwenyekiti wa taifa, Bw.James Mbatia ni mkakati wa kutaka nafasi hiyo ichukuliwe na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw.Zitto Kabwe.
Wakati hayo yakithibitishwa Dar es Saalam jana na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi wa jimbo la Kawe Bw.Hemed Msabaha, Bw. Zitto akijibu tuhuma hizo akiwa hospitalini India akipata matibabu alisema hana mpango wowote wa kuhama CHADEMA.

Alisema kila siku amekuwa akisema atakuwa  mwanachama wa chama kimoja tu cha siasa katika maisha yake yote na alikuwa mwanachama wa CHADEMA kutoka akiwa na umri wa miaka 16 na anamwomba Mungu kila siku afe akiwa ndani ya chama hicho.

Alisema anajua kuna watu wanapenda atoke CHADEMA kwa maslahi yao ya kisiasa wakimuona ni tishio kwao hivyo anawaambia kuwa ametumia nguvu nyingi kujenga Chadema na sitahama na kutaka waache kumzushia na kumjengea chuki mbele ya umma.

Bw. Zitto alisema hahusiki kwa lolote lile na yanayoendelea ndani ya NCCR mageuzi na wala hana sababu ya kuyajua.

"Mbunge wa Kasulu mjini ambaye alikuwa mwanachadema na kushinda Ubunge kwa sababu ya kutumia jina langu huko kwao Kasulu anaropoka (kama kweli kasema maneno hayo) na nitakapotoka Hospitali nitamtaka anithibitishie anayoyasema, vijana wanapojiingiza kwenye siasa za uwongo kama wazee wao ni hatari sana kwa nchi"

"Sihitaji kwenda NCCR ili kugombea Urais kwani chama changu ni kikubwa zaidi na kitanipa Urais kwa urahisi kuliko NCCR ambacho ni chama kisicho na rekodi yeyote ya kupigania maslahi ya nchi hata wakati kilipokuwa chama kikuu cha upinzani nchini".alisema Bw. Zitto.

Alisema katiba haimruhusu kugombea urais mwaka 2015 na hata kama ikibadilishwa na kumruhusu kugombea kwake kutategemea mwafaka ndani ya chama chake.

Alisema anayedhani kwamba nia yake ya kuwa Rais wa Tanzania ni ya kufa na kupona hamjui Zitto kwa sababu hafanyi siasa za kufa na kupona, anao uwezo wa kuwa rais bora maana anazo ajenda na anatoka chama bora, lakini pia yupo tayari kufanya kazi yeyote ile ambayo chama chake kitampa.

Wapo wanaishi kwa siasa za kumwaza Zitto na wamo kwenye vyama vyote vya siasa hapa nchini kwa vile anafanya kazi zake za ubunge kwa ufanisi na mafanikio makubwa na pia anafanya kazi zake za Uenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma kwa umakini mkubwa na anafanya kazi zake za uwaziri Kivuli wa Fedha katika hali ya kuridhisha sana.

Alisema maadui zake wa kisiasa wanatamani aanguke lakini kwa uwezo wa Mungu hataanguka.

Katika mkutano wa Bw. Msabaha alisema kuwa,Mei 30 mwaka huu alipigiwa simu na Mbunge wa kigoma Kusini Bw.David Kafulila na kumwambia kuwa wakazi wa Kigoma nao wanataka mwenyekiti wa chama cha siasa kutoka mkoa huo.

"Bw.Kafulila alinipigia simu huku akiwa na imani kuwa mimi ni mtu wa Kigoma mwenzake ningeweza kumuunga mkono kuhusu ombi la wakazi wa Kigoma kutaka mwenyekiti wa Chama cha Siasa kutoka mkoa huo kama ilivyo mikoa mingine"alisema Bw.Msabaha.

Alisema kuwa baada ya kumwambia hivyo alimuuliza kuwa mwenyekiti atakuwa nani,ndipo alipomjibu kuwa atakuwa Bw.Zitto ambapo tayari amekubali.

Alisema kuwa baada ya mazungumzo hayo Bw.Kafulila alisafiri kwenda nje ya nchi na baada ya kurudi alimwandikia ujumbe kwa njia ya simu ya mkononi kuwa tayari fungu limepatikana hivyo kilichobaki kumng'oa Bw.Mbatia na watu wa nje wameonyesha nia ya kusaidia .

"Baada ya kupata ujumbe ule niliimuuliza kwa kipindi hiki ambacho Bw.Zitto yupo Chadema Mwenyekiti atakuwa nani, ambapo alinijibu kuwa atakuwa yeye mwenyewe huku amkimsubiri Bw. Zitto" aliongeza.

Alisema kuwa Bw. Kafulila alimwambia kuwa mara baada ya Bw. Zitto kutoka Chadema, NCCR Mageuzi  kitakuwa na wanachama wengi kwani Bw.Zitto ataongoza kuiobomoa Chadema ataondoka na nusu ya wanachama hivyo hakitakuwa na nguvu tena.

"Unajuwa Bw.Zitto akiimega Chadema na wanachama wengine watatoka Chama cha Mapinduzi (CCM) hivyo ana imani chama hicho kitakuwa na nguvu.

Alisema kuwa, Bw.Kafulila alimwambia kuwa kuna baadhi ya wanachama wa CCM wanataka kuanzisha chama chao ila kutokana na ugumu uliopo katika kuanzisha chama watajiunga NCCR Mageuzi.

"Unajuwa kuna wanachama wa CCM wanataka kujiondoa na chama hicho kuanzisha chama chao ila kutokana na ugumu uliopo katika kuanzisha chama watahamia NCCR hivyo chama hicho kitakuwa na nguvu na kitachuana na CCM"alisema Bw.Msabaha.

Hata hivyo Bw.Msabaha alisema kuwa Chama hicho hakipo katika hali tete kama watu wanavyozungumza na kuhusu kumng'oa Bw.Mbatia suala hilo  halipo ni maneno ya nje na ni mtu mmoja mwenyewe ambaye anatumiwa na watu kufanya hivyo.

Pia alisema kuwa Chama chao kina utaratibu na katiba ambapo mtu akikutwa na kosa ambalo likathibitika anaweza kufukuzwa uanacahama hivyo suala la Bw.Kafulila lipo katika uchunguzi.

Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo amewataka wanasiasa kutoka ndani na nje ya chama hicho kuacha kuzungumzia kesi ya Mbunge wa Kawe Bi.Halima Mdee na Bw.James Mbatia kwani kesi hiyo ipo mahakamani waachie ifanye kazi na wasiingilie uhuru.

Katika sakata hilo pia Mbunge wa Kasulu mjini Bw. Moses Machali amemshutumu vikali Bw. Kafulila kwamba anatumiwa na Naibu Katibu mkuu wa Chadema Zitto Kabwe kukivuruga chama hicho.

Mbunge huyo wa Kasulu anadai kuwa lengo kubwa la Kafulila ni kumwondoa mwenyekiti wa chama hicho Bw. Mbatia ili yeye awe mwenyekiti.

No comments:

Post a Comment