Monday, November 14, 2011

Moto wa Katiba Mpya kuwaka bungeni leo

 Na Salim Nyomolelo

*Wanaharakati: Kutachimbika kama utapitishwa
*Watishia kuhitisha maandamano nchi nzima
*Walemavu wauponda, wasema si rafiki
*Wabunge nao wajipanga kuonesha uzalendo

WAKATI Bunge la Tanzania linatarajia kupokea, kujadili na kupitisha muswada wa sheria ya jinsi ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya, wanaharakati wanaojipambanua kama Jukwa la Katiba Jijini Dar es Salaam wamekuja juu na kutangaza kufanya maandamano ya nchi nzima iwapo itasomwa kwa mara ya pili kama ilivyopangwa na serikali.


Wakati wanaharakati hoa wakisema hayo Mjini Dodoma wabunge nao wamejipanga kusimamia kile walichodai kuwa ni haki ya umma kwa kuukataa iwapo itakuwa na mapungu kama ile waliokataa mwezi Aprili mwaka huu.

Katika mdahalo huo uliojumuisha makundi mbalimbali ya kijamii, watu wenye ulemavu kwa upande wao walidai kutengwa na muswada huo na kueleza kuwa si rafiki kwao.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Bw. Deus Kibamba, akizungumza katika mdahalo huo ulioandaliwa katika jengo la Ubungo Plaza Dar es Slaam jana, alisema kiini cha madai yao ni kutaka muswada huo usomwe bungeni kwa mara ya kwanza na sio mara ya pili ili kuwapa nafasi wananchi kuusoma na kutoa maoni yao kwanza.

"Kwa leo muda wetu umeishia hapa, sasa nataka nitoe majumuisho kwa yote tuliyozungumza hapa, woga ni kitu cha hoja, tutawaongoza kwa chochote mtakachoamua, maandamano ya Katiba itakuwa balaa, hakuna Polisi,Jeshi, Mgambo, viongozi wala wanasiasa watakaozuia.

Ukisomwa kwa mara ya pili tutaandaa maandamano yasiyo na kikomo kwa kufanya mambo makubwa na hakuna mtu atazuia,"alisema Bw. Kibamba.

Alisema muswada huo uliposomwa na kukataliwa bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Aprili mwaka huu ulitakiwa kuandaliwa upya kisha kufuata taratibu zote badala ya kuurekebisha kisha kuendelea na hatu ya pili kana kwamba ulikubalika wakati hali ni tofauti.

Akichangia hoja katika mdahalo huo, Bi. Christina Kamuli, ambaye pia ni mjumbe wa Jukwaa la Katiba alisema muswada huo ulitakiwa kusomwa bungeni kwa mara ya kwanza kwa kuwa ushirikishwaji uliotolewa kwa wananchi haujitoshelezi.

Awali katika vikao vya Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala ilipokutana katika ofisi ndogo za bunge Jijini Dar es Salama pia baadhi ya wajumbe walalamika na kuwaambia waandishi wa habari kuwa walipewa muda mfupi kuupitia muswada huo.

Katika maoni yao baadhi ya wajumbe hao walisema walipewa siku mbili tu kabla ya kikao chao wakati taratibu walitakiwa wapewe wiki mbili kabla ili waweze kuupitia na kutoa mapendekezo yao.

Alitaja moja ya upungufu mkubwa kwa katiba ya sasa ambayo lazima ungaliwe kwa umakini mkubwa katika Katiba Mpya kuwa na uundwaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuonya kuwa kama wananchi hawatashirikishwa kwa undani kipindi hiki cha awali haitawezekana kushirikishwa katika ngazi inayofuata.

Naye Prof.Josephat Kanywanyi, ambaye pia ni Manasheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alipinga muswada huo kusomwa kwa mara ya pili bungeni kwa kile alichodai kuwa ni idadi kubwa ya watanzania kutouna hadi sasa.

Alisema ni lazima watanzania wapate nafasi ya kutosha kuupitia muswada huo na kutoa mapendekezo au maoni yao ili yaingizwe katika mchakato wa Uundwaji katiba kwa kuwa wanataka kupata unafuu wa maisha yao katika kipindi cha miaka 50 ijayo.

"Ni lazima watanzani watoe madukuduku yao wanavyotaka muswada uwe",aliseam prof.Kanywanyi.

Alirejea tena hoja ya muswada huo kumpa rais mamlaka makubwa na kutaka hadidu rejea za muswada huo kuwekwa wazi zaidi ili kila mtu azijue mapema kabla ya kazi kuanza.

"Katika muswada huo rais ni kila kitu, uteuzi yeye, hadidu rejea yeye na sheria ipo kwa ajili ya watu na sio watu wapo kwa ajili ya sheria,"alisema.

Prof Kanywanyi alisema muswada unatakiwa rais awe muidhinishaji na mratibu na ashiriki katika kutoa maoni yake kama mtanzania na sio kufanya maamuzi kwa kile alichodai kuwa hali ikiwa hivyo katiba hiyo haitakuwa ya Tanzania bali ya mtu mmoja.

Naye mwakilishi wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Bw.Hezron Kaaya, alidai Waziri wa Katiba na Sheria aliidhinisha muswada huo kwa kile alichokiita kuwa ni kuwafanya viongozi kuishi vizuri hata baada ya kustaafu.

"Tukiharibu katika maandalizi ya kuipata Katiba mpya, tutapata katiba mbovu na watanzania tuelewe kuwa tunao viongozi ambao ni wanafiki ambapo kwao 2X2 kwao ni 5 kwa kujipendekeza kwa rais",alisema Bw.Kaaya

Aliwashauri wabunge kutokubali kile alichoita kuwa ni kuburuzwa kwa kusema ndio kwa jambo ambalo hawalifahamu kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuleta tatizo kubwa baadaye.

Kwa upande wake mwanaharakati aliyejitambulisha kwa jina la Catherine Malila,alidai iwapo muswada huo utasomwa kwa mara ya pili na kupitishwa na bunge wanawake watatangulia mbele barabarani katika maandamano ya kuupinga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bi.Ussu Malya, alienda mbali zaidi na kueleza kuwa katiba ya sasa haitoi dira ya siasa nchini na muktadha wa mwanamke hasa wa kijijini kwa kile alichodai kuwa ni kukosekana kwa kipengere kinachoelezea kubomoa mfumo dume hivyo mchakato wa katiba Mpya lazima izingatie suala hilo.

"Mfumo Dume na Kibepari ndani ya Katiba ya sasa haimpi haki mwanamke katika maamuzi, tunahitaji katiba inayotoa haki sawa kati ya mwanamke katika kufanya maamuzi,hadidu za rejea zieleze hivyo mapema kabla ya hatua ya pili kuanza",alisema Bi. Malya.

Naye mchangiaji mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Malia Chale, aliyejipambanua kuwa ni mwakilishi kutoka Kituo cha haki za watu wenye ulemavu, alisema muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza kwa kuwa haujawashilikisha watu wenye ulemavu katika mchakato wote.

"Muswada huo ulichapishwa katika gazeti la serikali lakini sio katika nukta nundu (alama zinazosomwa na watu wenye ulemavu wa kuona) ili na sisi watu wenye ulemavu tuusome," alisema.

Alisema kundi la watu wenye ulemavu halikubali muswada huo usomwe kwa mara ya pili kwa kile alichoeleza kuwa sio rafiki kwao kutokana na kutowajali.

Alifafanua kuwa kipindi cha upigaji kura huwa wanashirikishwa tena kwa kusogezewa vifaa kwa kutambua udhaifu wao lakini walishangaa kutoshirikishwa katika mchakato wa Sheria ya kuunda Tume ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya hivyo kuonekana kuwa kundi hilo sio muhimu.

Alihoji pia sababu za muswada huo kutoweka wazi nafasi ya wanasiasa na kudai kuwa wakati wa kufunika mambo umepitwa na wakati na kwamba watanzania wanataka kila kitu kiwekwe wazi.

Muswada huo ni mtihani mwingine mgumu kwa wabunge wa Tanzania kwa kuwa baadhi ya wananchi wameonekana kutoa kauli zinazowaweka pagumu wawakilishi hao kutoa msimamo. Bunge linatarajiwa kuwa na mjadala mkali juu ya muswada huo baada ya ile ya Sheria mpya ya Manunuzi ya umma.

Hata hivyo baadhi ya watanzania wamekuwa wakijichanganya kuhusu Sheria ya kuunda Tume itakayokusanya maoni ya jinsi ya kuunda Katiba Mpya na Katiba yenyewe huku baadhi ya watu wakitoa maoni kana kwamba kinachotakiwa kwa sasa ni kutoa maoni kuhusu Katiba yenyewe hatua ambayo bado haijafikiwa.

Tayari Rais Jakaya Kikwete, amewahakikishia Watanzania kuwa hatamaliza muda wake mwaka 2015 bila kuwaachia Katiba Mpya na kuweka wazi kuwa kazi hiyo itakamilika mwaka 2014.

No comments:

Post a Comment