Wednesday, November 16, 2011

Ghorofa la mbunge labomolewa

   MAMLAKA ya Mji Mkongwe, Zanzibar, imebomoa ghorofa la kigogo katika eneo la Malindi, baada ya kukiuka maelekezo yaliyotolewa katika kibali cha ujenzi.

Jengo la ghorofa tatu lililobomolewa linamilikiwa na mwakilishi wa Muyuni,  ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Ayuob.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe, Issa Sarboko Makarani, akizungumzia ubomoaji huo, alisema wamelazimika kuchukua hatua kwa kuwa kibali kinaruhusu ujenzi wa ghorofa moja, hivyo inashangaza kuona kumejengwa ghorofa tatu na ujenzi unaendelea.

Issa alisema awali, baada ya kuona ujenzi wa nyumba hiyo unakiuka kibali cha ujenzi, mamlaka ilitoa agizo la kusitisha ujenzi lakini lilipingwa na mafundi waliendelea na ujenzi.
Mkurugenzi huyo alisema kinachoendelea sasa ni ubomoaji wa ghorofa ambazo hazikuwemo katika kibali na ramani ya ujenzi wa nyumba hiyo.
Alisema mamlaka imekuwa ikieleza na kuweka wazi kuhusu ujenzi katika eneo la Mji Mkongwe, lakini kesi kadhaa zimefunguliwa kupinga taratibu hizo.

Issa aliwataka wananchi watambue Mji Mkongwe wa Zanzibar ni mmoja kati ya urithi wa kimataifa, hivyo hawana budi kudumisha yote yanayoupa hadhi, ikiwemo kuendeleza makazi kama itakavyoelekezwa na mamlaka husika.

Mkurugenzi huyo pia aliwataka wananchi waache ubishi katika kutekeleza taratibu zinazotolewa na taasisi husika katika kuuenzi Mji Mkongwe.
Alisema endapo wananchi wataendelea kujenga na kupuuza maagizo ya mamlaka husika, hasara wanazoweza kuzipata ni kubwa, ikiwemo kubomolewa nyumba zao.

Katika kufikia utunzaji bora wa Mji Mkongwe, alisema mamlaka ipo tayari kutoa elimu na maelekezo kwa wananchi au taasisi yoyote kuhusu namna ya utunzaji wake.
Hatua ya mamlaka hiyo imechukuliwa siku chache baada ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, kusema tatizo la ardhi ni kubwa na lenye mambo mazito.
Alisema baada ya muda wananchi watasikia matokeo yake kwa suala la ardhi, kwani ndiyo jambo la pili kwa umuhimu katika ufuatiliaji wake.

No comments:

Post a Comment