Thursday, November 24, 2011

SMZ yaahidi uhuru wa habari

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema itahakikisha inafungua milango zaidi ya uhuru wa vyombo vya habari kwa ajili ya wananchi kupata taarifa mbalimbali kwa mujibu wa Katiba.

Hayo yalisemwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa sherehe
za kukabidhiwa leseni ya matangazo kwa kituo cha StarTimes cha China visiwani hapa.

Maalim Seif alisema Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inatambua kuwepo kwa umuhimu wa
kila raia wa Zanzibar kupata taarifa mbalimbali za habari ndani na nje ya nchi kwa lengo la kukidhi matakwa ya Katiba.

“Kwa ajili ya kukidhi matakwa ya Katiba, ndiyo maana tumeamua kufungua milango na
kuzikaribisha kampuni mbalimbali za nje na ndani ya nchi kuwekeza Zanzibar katika sekta ya mtandao wa kisasa wa mawasiliano,” alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.

Hata hivyo, alisisitiza na kutoa tahadhari kwamba kampuni zote zitakazokuja kuwekeza katika sekta ya habari ya mawasiliano, zinatakiwa kwanza kuzingatia maadili na utamaduni wa
wananchi wa Zanzibar.

Alisema Serikali haitakubali kuona utamaduni na silka za wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba unapotoshwa kwa kisingizio cha uhuru wa vyombo vya habari pamoja na utandawazi wa teknolojia ya mawasiliano.

“Hayo ndiyo masharti yetu makubwa katika uwekezaji wa sekta ya habari na mawasiliano nchini... utamaduni lazima uzingatiwe na kulindwa kwa nguvu zote kwani ndiyo utambulisho wa wananchi wa Zanzibar,” alisema.

Kampuni ya StarTimes kutoka China imepewa leseni ya kuendesha shughuli za televisheni Zanzibar na kuwa kampuni ya kwanza ya kigeni kupata fursa hizo.

Kampuni hiyo imepewa leseni ambayo itaiwezesha kuwekeza katika mitambo ambayo hatimaye itagawa mawimbi kwa kampuni za redio na televisheni nchini.

No comments:

Post a Comment