Thursday, November 24, 2011

Gamba gumu CCM


WATUHUMIWA WAGOMA KUJIUZULU,JK AHOJI UVCCM WALIKOPATA FEDHA
Neville Meena, Dodoma
UTEKELEZAJI wa mpango wa CCM uliolenga kuwashinikiza watuhumiwa wa ufisadi kuachia nafasi zao za uongozi ndani ya chama hicho, umechukua sura mpya na sasa Kamati Kuu (CC) inaomba ipewe kibali cha kuwachukulia hatua zaidi wale ambao wamegoma kujiuzulu.Juzi, katika kikao chake mjini hapa, CC iliazimia kuomba idhini ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ili ifanye kazi hiyo baada ya kuwepo ukimya ambao unaashiria kutokuwepo viongozi na makada ambao wako tayari kujiuzulu nyadhifa zao kwa hiari.

Tangu kupitishwa kwa mpango huo maarufu kwa jina la kujivua gamba katika kikao cha NEC kilichopita cha Aprili mwaka huu, ni kada mmoja tu, Rostam Aziz aliyechukua hatua za kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Igunga na ujumbe wa NEC, lakini wengine wamekuwa kimya hadi sasa.

Katika kikao cha Aprili NEC hiyo ya CCM ilipitisha maazimio 26 lakini kubwa ni lile lililokuwa likihimiza vita dhidi ya ufisadi kuendelea na kutoa mwito kwa watu wanaotajwa na jamii kuhusika na ufisadi ambao wako ndani ya chama kujitathmini kisha kuchukua hatua za kuachia madaraka waliyo nayo.

Sehemu ya mwisho ya azimio hilo inasomeka: “Wasipoachia madaraka chama kiwachukulie hatua mara moja.”

Mmoja wa wajumbe wa CC ambaye ameomba jina lake kuhifadhiwa alisema: “Tunawaomba NEC waturuhusu jambo hili tulifanyie kazi sisi (CC) na litafanyiwa kazi kupitia taratibu za kawaida za chama kwa kuzingatia kanuni na taratibu za maadili za chama hicho.”

Kubadilika kwa utaratibu wa kuwashughulikia watuhumiwa wa ufisadi, kulipokewa kwa shangwe na wafuasi wa watuhumiwa hao ambao wanasema kulikuwa na ajenda ya siri, kubwa likiwa ni vita ya urais wa 2015.

Hata hivyo, kada mwingine ambaye yuko karibu wa vigogo wa chama hicho alisema: “Hivi sasa hali itakuwa mbaya zaidi kwa watuhumiwa, tunakokwenda si hiari tena itakuwa ni lazima ikiwa chama kitawapata na hatia.”

“Ujue azimio la kwanza lilikuwa na pande mbili, kwanza ni watuhumiwa hao kujipima wenyewe kisha kuchukua hatua, lakini pili ni upande wa chama, sasa ukomo wa upande wa kwanza ambao ni kuchukua hatua wenyewe umekwisha, sasa ni zamu ya upande wa pili ambao ni wa chama,” alisema kada huyo ambaye pia ni mshiriki wa vikao vya uamuzi ndani ya CCM.

Makatibu wapya
Halmashauri ya CCM iliyoanza mkutano wake jana, ilifanya mabadiliko ya makatibu wa chama hicho katika mikoa sita.Walioteuliwa ni Joyce Masunga, Mohamed Nyawenga, Pazi Mamulima, Zainab Shomari, Abdallah Mihewa na Rahel Ndegeleki ambao watapangiwa vituo vya kazi hivi karibuni.

Habari kutoka katika kikao cha Kamati Kuu zinasema kwamba imebariki pendekezo la kumvua madaraka kiongozi mmoja wa ngazi za juu baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kubadili orodha ya matokeo ya kura za madiwani wa Viti Maalumu bila kushirikisha vikao husika.

Kigogo huyo alitiwa hatiani kuchakachua orodha ya madiwani iliyowasilishwa Tume ya Tiafa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuondoa jina namba mbili katika mtiririko wa orodha hiyo na kuliweka chini, hivyo kumkosesha mmoja wa makada wa chama chake nafasi ya kuwa diwani.

Kikwete anena
Kikao cha NEC kilianza jana saa 5:00 asubuhi kwa Rais Kikwete kuwatoa hofu wajumbe akisema hakuna kitakachoharibika. Mara baada ya kuingia, Rais Kikwete aliwasalimu wajumbe akisema: “Jamani hamjambo …. mmelala salama?” Baada ya wajumbe kujibu ndiyo aliongeza:

“Mbona nimeambiwa kwamba wajumbe wengine hamjalala vizuri, mmelala na hofu tu, CCM ni chama kikubwa, kwa hiyo jamani tulieni hapa hakuna jambo litakaloharibika, watu msiwe na hofu,” alisema kisha kutamka kwamba kikao hicho kimefunguliwa rasmi na kuwataka waandishi wa habari kutoka ndani ya ukumbi wa mikutano.

Kauli ya Kikwete ilikuwa ni kama mwangwi wa yaliyotokea juzi usiku baada ya kumalizika kwa kikao cha CC, kwani wapambe wa makundi mawili hasimu ndani ya chama hicho yalikuwa yakihaha kushawishi kuungwa mkono na wajumbe wakati wa vikao vya NEC.

Kati ya saa saba na nane usiku wa kuamkia jana, wapambe wa makundi hayo na mmoja kati ya makada hao alisikika akisema kuwa: “Ujue sikulala kabisa na sasa naingia kwenye NEC, fitina ilikuwa kubwa sana jana (juzi) usiku, lakini tutashinda tu.”

Kundi la makada wanaojipambanua kuwa wapambanaji wa ufisadi walikuwa wakihaha kushawishi wajumbe wa NEC kukataa uamuzi wa suala la kujivua gamba kurejeshwa CC, wakati kundi la pili lilikuwa likishawishi wajumbe kusimama kidete na kuunga mkono pendekezo hilo.

Habari zilizopatikana jana jioni zinadai kuwa, jana NEC haikuwa imejadili suala lolote kuhusu kujivua gamba na kwamba hata mmoja wa wajumbe ambaye amekuwa akitajwa katika suala hilo, Edward Lowassa alipotaka kulizungumzia aliambiwa asubiri wakati mwafaka wa ajenda husika.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu pendekezo hilo alisema: “Jamani, kikao hiki bado kinaendelea, kama kuna jambo lolote mimi niliwaahidi kwamba niko tayari kuwaambia.”

“Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote zaidi ya yale niliyowafahamisha leo (jana) mchana na ujue kwamba yapo mambo mengi ambayo ili kwenda kwa umma lazima yapate kibali cha NEC, vinginevyo nitakuwa navunja taratibu,” alisema Nape.

Kombora UVCCM
Katika hatua nyingine, kundi la viongozi na marafiki wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) lililopo Dodoma, jana lilitaharuki baada ya kupokea taarifa za kurushiwa makombora, huku Rais Kikwete akiwazodoa kwa kuwaambia: ‘Msitutishe,’ ishara ya kukerwa na taarifa kwamba vijana hao walitishia kuhamia Chadema ikiwa Umoja wao utavunjwa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao cha CC kilichomalizika juzi usiku zinasema, ajenda kuhusu UVCCM ni kama haikuwa rasmi lakini baada ya kuibuliwa na Nape ilisababisha Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Benno Malisa kusakamwa ipasavyo na kutishwa kwamba hatima yake kisiasa inaweza kuwa mbaya.

“Yule bwana mdogo (Benno) alipata wakati mgumu sana, maana wale wazee walimshughulikia ipasavyo, alijaribu kujitetea lakini haikusaidia, kweli nilimwonea huruma sana maana hakuwa na mtetezi mle ndani,” kilisema chanzo kingine kutoka ndani ya CC.

Taarifa hizo ziliendelea kudai kuwa Nape aliomba kikao hicho kimpe majibu ya kutoa kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa wakimwuliza kuhusu suala hilo ambalo alisema hakuwa na majibu.

“Nimeambiwa UVCCM viongozi wa mikoa na baadhi ya wilaya wako hapa, mwenyekiti naomba nipate majibu nisaidiwe katika hili, kama ni Baraza Kuu linakutana nifahamu na kama kuna mkutano mwingine nijue pia, lakini hali hii inaniweka katika wakati mgumu mimi kama mwenezi,” alinukuliwa Nape na chanzo chetu ndani ya CC.

Maelezo hayo yalisababisha Benno kusimama kutoa utetezi ambao hata hivyo, haukusikilizwa na hapo wajumbe wawili, Mawaziri, William Lukuvi na Steven Wassira kila mmoja kwa wakati wake, aliushambulia umoja huo.

Inadaiwa kuwa Rais Kikwete ndiye aliyegongelea msumari wa mwisho pale aliponukuliwa na mtoa taarifa wetu akisema: “Mnataka kututisha, msitutishe hata kidogo maana nasikia kwamba mnataka kwenda Chadema, nendeni hata kesho, au mnasubiri tuuvunje ndiyo muondoke!”Kadhalika Rais alinukuliwa akihoji vijana hao walikopata fedha zinazowawezesha kukaa hapa kwa muda wote huku akiwakumbusha kwamba CCM hakiwezi kuyumba ikiwa kitawatimua kwani kimewahi kufanya hivyo kwa viongozi wa ngazi za juu.

Pamoja na hali hiyo, viongozi wengi wa UVCCM wa mikoa na wilaya mbalimbali nchini bado wapo Dodoma na baadhi yao walisema huenda wakatoa tamko baada ya kikao cha NEC kumalizika.

No comments:

Post a Comment