Saturday, November 19, 2011

Uranium iwanufaishe Watanzania -Jaji Bomani

 
TANZANIA imeshauriwa kujiridhisha kuhusu faida zitakazotokana na madini ya uranium kabla ya uchimbaji kuanza katika maeneo mbalimbali nchini. Sambamba na hilo, imetakiwa kuangalia na kupima athari za mradi huo ambao ni muhimu katika kukuza uchumi. Rai hiyo ilitolewa jana mjini Dar es Salaam na Jaji mstaafu, Mark Bomani, wakati akifungua warsha ya siku moja kwa wadau wa madini hayo, wakiwemo wale wa kimataifa. Jaji Bomani alisema madini hayo ni sehemu ya urithi wa Tanzania, na kwamba yanapaswa kuwaneemesha Watanzania wenyewe.

"Ni vyema ikafanyika tathmini ya kina kujua faida na hasara za kuchimba kabla ya kuanza kuchimba uranium," alisisitiza Jaji Bomani.Kwa mujibu wa Jaji Bomani, madini hayo yakichimbwa na kulenga kuendeleza uchumi wa Tanzania, yanaweza kuwa eneo muhimu katika kuhakikisha hali ya maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa zinaboreka. "Tunatambua jinsi madini haya yanavyoweza kutatua tatizo la nishati ya umeme, ambayo kwa kiasi kikubwa inazorotesha uzalishaji na ukuaji wa uchumi wetu," alisema.

Hata hivyo, alisema ni vyema pia kutazama changamoto mbalimbali zinazoweza kuibuka kutokana na uchimbaji wa madini hayo, hususan madhara ya kiafya kwa jamii zinazozunguka maeneo ya machimbo.
Alisema katika baadhi ya nchi zinazochimba na kurutubisha madini hayo kama vile Japan, kumekuwa na changamoto ya ulipukaji wa vinu vyake na kusababisha madhara kwa jamii, hivyo ni muhimu kubaini hilo na kuchukua tahadhari kabla ya uchimbaji kuanza. Hata hivyo, miongoni mwa wadau waliohudhuria warsha hiyo, walisema licha ya madhara yanayoweza kutokea kutokana na madini hayo, bado si makubwa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu wanaojaribu kuwajengea hofu wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Saveli Maketta, alisema baadhi ya watu huenda wanatumiwa na nchi za nje ili kuwatia hofu Watanzania wasitoe ushirikiano katika mradi wa uchimbaji wa madini hayo.
"Endapo tutachimba madini haya, tutakuwa nchi ya tatu barani Afrika na saba duniani, huku tukiziacha mbali hata nchi kubwa... huenda baadhi ya nchi hazipendi hali hii itokee, na hivyo kutoa vitisho kwa kisingizio cha madhara ya kibinadamu," alisema Maketta.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Uranex ya Marekani inajihusisha na utafiti wa madini hayo, Godwin Nyero, alisema madhara yatokanayo na madini hayo hayawezi kupatikana kwa urahisi, na kwamba hatua za utafutaji na uchimbaji hufanyika kwa tahadhari kubwa.
Nyero alisema wananchi wa maeneo kama vile Manyoni na Namtumbo, ambako madini hayo yamegunduliwa, licha ya kuishi nayo kwa muda mrefu, bado wapo salama, huku wakinywa maji yaliyo katika ardhi iliyobeba madini hayo.

Utafiti uliofanywa umebaini kuwepo kwa hazina kubwa ya madini hayo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma na Manyoni mkoani Singida.
Uchimbaji wa madini hayo ambayo ni moja ya nyenzo muhimu katika uzalishaji wa nishati mbalimbali, unatarajiwa kuanza mwaka 2014.

No comments:

Post a Comment