Thursday, November 17, 2011

Maranda na wengine waunganishwa kesi ya EPA

 VIGOGO wawili wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),  walipandishwa tena kizimbani jana, kuunganishwa katika kesi ya kujipatia sh. bilioni 5.9 kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), kwa njia ya udanganyifu. Mbali na vigogo hao ambao ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Madeni, Esther Komu na Kaimu Katibu wa benki hiyo, Bosco Kimela, mshitakiwa mwingine aliyeunganishwa ni mfanyabiashara Rajabu Maranda.

Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuunganishwa kwenye kesi inayowakabili ndugu wawili Ajay Somani na Jai Somani.
Esther, Kimela na Maranda,  wanakabiliwa na kesi nyingine za EPA mahakamani hapo.
Maranda alifika mahakamani hapo akitokea gerezani anakotumikia kifungo cha miaka mitano jela, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujipatia sh. bilioni 1.08  kupitia akaunti ya EPA mali ya BoT.
Mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, Wakili wa Serikali Mkuu Fredrick Manyanda, alidai shauri hilo linakuja kwa usikilizwaji wa awali.
Hata hivyo, aliomba kubadilisha hati ya mashitaka kwa kuwaunganisha Maranda, Esther na Kimela.
Baada ya kukubaliwa kwa ombi hilo, Manyanda aliwasomea mashitaka ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kujipatia ingizo na kuisababishia mamlaka husika hasara.
Maranda, Ajay, Jai  wanadaiwa kuwa tarehe tofauti Desemba mwaka 2004, na Mei 2005, sehemu zisizofahamika Dar es Salaam, walikula njama ya kufanya kosa la jinai la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Maranda anadaiwa Desemba 15, mwaka 2004, Dar es Salaam kwa makusudi na kwa nia ya kurubuni, alighushi hati ya kuhamisha fedha kati ya Philip Sceman wa Societe Alsacenne Construction De Machines Textiles  ya Paris, Ufaransa na Maulidi Kasasa wa Liquidity Services Ltd, kuonyesha kuwa Kasasa alipewa deni la sh. 5,912,901,643 na kampuni hiyo ya Ufaransa.

Pia, Maranda anadaiwa Agosti 30, 2005, katika benki ya Baroda Tanzania Limited, aliwasilisha hati hiyo ya kughushi.

Maranda, Ajay na Jai wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Septemba 2 na Desemba 13, 2005, mjini Dar es Salaam, walijipatia sh. bilioni 3,975,820,000 mali ya BoT baada ya kudai kuwa Kasasa alipewa deni hilo na kampuni ya Ufaransa.
Maranda anadaiwa tarehe hizo pia alijipatia ingizo la sh. 1,937,081,643 kutoka BoT.
Washitakiwa Esther na Kimela wanadaiwa wakiwa waajiriwa wa BoT, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Madeni na Kaimu Katibu wa benki kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kiwango cha kawaida, waliisababishia hasara BOT ya sh. bilioni 5,912,901,643.
Washitakiwa hao walikana mashitaka.
Esther na Kimela waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kutia saini bondi ya sh. bilioni mbili na kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaotia saini bondi ya sh. bilioni 1.5.
Kwa upande wa Maranda ambaye masharti yake ya dhamana ni kama ya Ajay na Jai, alishindwa kutimiza masharti kwa kuwa hakuwa na wadhamini.
Akiahirisha shauri hilo, Hakimu Katemana alisema Ajay na Jai wanaendelea na dhamana huku Esther na Kimela wakiachiwa kwa dhamana.
Alisema kesi itatajwa Desemba mosi mwaka huu na itasikilizwa mfululizo kuanzia Januari 16 hadi 20, mwakani.

No comments:

Post a Comment