Monday, November 28, 2011
Posho za wabunge zapanda kimyakimya
ZAPANDA KUTOKA SH70,000 HADI 200,000, NI ZAIDI YA ASILIMIA 150
Fredy Azzah
HUKU mjadala wa kufutwa au kwa posho za wabunge na watumishi wengine wa Serikali ukiwa umefifia, posho za vikao (sitting allowance) za wabunge zimepanda kutoka Sh70,000 kwa siku hadi Sh200,000, imefahamika.
“Zimeongezeka kutoka Sh70,000 mpaka 200,000, wameanza kulipwa Bunge lililopita hili ni ongezeko la karibu mara tatu, yaani asilimia 154,” kilieleza chanzo chetu kutoka ndani ya Ofisi za Bunge.
Kutoka na ongezeko hilo, kwa sasa kila mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 ikiwa ni posho ya kujikimu (perdiem) anapokuwa nje jimbo lake, posho ya vikao (sitting allowance) Sh200,000 na mafuta ya gari Sh50,000 kila siku, ambazo jumla yake ni Sh330,000 kwa siku.
Kutokana na ongezeko hilo, Bajeti ya Bunge kwa ajili ya posho za vikao vya wabunge imepanda na kufikia Sh28 bilioni kwa mwaka.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu siyo msemaji wa wabunge, bali Ofisi ya Bunge.
“Ni nani kawapa hizo taarifa bwana, au ni vyanzo vyenu vya habari?” alihoji Dk Kashililah.
Baada ya kuelezwa kuwa taarifa hizo zimetoka kwenye vyanzo vyetu vya kuaminika alisema “Hao wana utaratibu wao bwana, labda mtafute Spika ndiye msemaji wa Wabunge.”
Juhudi za kumpata Spika, Anne Makinda kutoa ufafanuzi wa suala hili, hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita wakati wote bila kupokewa hata pale alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu (sms) hakujibu. Hata simu zote za Naibu wake, Job Ndugai hazikupatikana.
Hata hivyo, Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na wabunge kuwa wanalipwa mishahara midogo kulingana na kazi wanayofanya.
Alisema endapo wawakilishi hao wa wananchi wangekuwa wanalipwa mishahara inayolingana na kazi wanayofanya, kusingekuwa na sababu ya kuongezeka kwa posho hizo.
“Ninachosema mimi, siyo wabunge peke yao, lakini watumishi wote wa umma wanalipwa mishahara midogo sana mimi binafsi sitegemei posho za Bunge, kabla ya kuingia bungeni nilikuwa nimefanya kazi kwa miaka 14 na nilikuwa napata mshahara mzuri tu,” alisema Filikunjombe.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema amezisikia taarifa hizo za kuongezeka kwa posho lakini siyo kwa undani. Hata hivyo alisema hakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumza suala hilo.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema walivyokuwa wakipinga posho hizo wakati zilivyokuwa Sh70,000 waandishi wa habari walichukua suala hilo kama ajenda ya Chadema, hivyo kupandishwa kwa posho hizo ni matokeo ya watu kuwapuuza walivyokuwa wakizipinga.
“Msimamo wetu sisi tulishautoa tangu wakati posho zikiwa Sh70,000 wakati sisi tukipinga hizi posho waandishi wa habari na Watanzania mlichukulia suala hili kama ajenda ya Chadema, sisi wenyewe tupo wachache bungeni, tulichotaka ni kuonyesha jinsi fedha za Watanzania zinavyotumika vibaya,” alisema na kuongeza:
“Achilia mbali hizo 200,000 za wabunge kuna watu huko serikalini wanalipwa mpaka Sh400,000 au Sh1 milioni kwa siku nyie ulizeni.”
Alipoulizwa kama amechukua posho hiyo ya Sh200,000 alisema hajafanya hivyo kwa sababu hazifuatilii.
“Sijui hata kama zimeanza kulipwa au la kwa sababu huwa sizifuatilii na haka kama suala la posho hilo zilijadiliwa wakati wa vikao vya mwanzo mimi sikuwepo kwa sababu tulikuwa kwenye kesi yetu Arusha na bungeni tulikuja mwishoni wakati wa Muswada wa Katiba,” alisema Mbowe.
Ongezeko hili la posho za wabunge limekuja wakati Watanzania wakiendelea kuishi kwenye maisha magumu yanayochangiwa na mfumuko wa bei ambao mpaka mwisho mwa Oktoba ulikuwa umefikia asilimia 17.9.
Pia ongezeko hili limekuja wakati Watanzania wakiwa na matumaini ya posho hizi kupunguzwa baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangaza bungeni kuwa Serikali imekubali pendekezo la kutafakari na kuziangalia upya posho mbalimbali wanazolipwa wabunge na watumishi wote umma.
Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali alisema kuwa hawezi kuzungumza chochote juu ya posho hizo kwa kuwa hajapata barua rasmi juu ya kupanda kwake.
“Sijapata barua yoyote, nikiuliza na kupata majibu kwa wahusika nitakuwa na uhakika na nitakupa maoni yangu na msimamo wangu vizuri kabisa, lakini kwa sasa siwezi kusema chochote,” alisema Mkosamali.
Juni 7, mwaka huu Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Zitto Kabwe, aliwasilisha barua Ofisi ya Bunge akikataa posho akisema watumishi wa Serikali na wabunge, hawastahili kulipwa posho wanapohudhuria vikao rasmi vya uwajibikaji wao wa kawaida.
Zitto alisema posho hiyo haistahili kulipwa kwake, wabunge wengine wala watumishi wa umma kwa kuwa kuhudhuria vikao ni sehemu ya kazi zao.
Alisema kitendo cha Waziri Mkuu kueleza kuwa watatafakari na kuangalia upya na kwamba suala la posho ni sera ya taifa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ni ishara ya kiongozi huyo wa juu kukubali wazo la Chadema na safari ya kufuta posho hizo.
Awali, mara baada ya Chadema kutangaza msimamo huo, Spika Makinda alipinga uamuzi wa kususia posho akisema suala hilo lipo kisheria na kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kuamua kuliondoa.
Alisema wabunge wa Chadema wataendelea kulipwa posho za vikao kupitia akaunti zao za benki na watatakiwa kusaini fomu ya mahudhurio ya Bunge, vinginevyo watajiweka katika wakati mbaya.
Hata hivyo, akihitimisha hoja za wabunge katika hotuba yake ya makadirio ya matumizi ya ofisi yake na zilizo chini yake juzi, Pinda alisema suala la posho lipo kwenye mchakato wa kuangaliwa upya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment