Jeshi la Kenya limewatahadharisha wananchi wa Kenya kutowauzia wapiganaji wa al-shabab punda kwa maelezo kuwa wanatumika kusafirishia silaha.
Msemaji wa Jeshi hilo amesma makundi makubwa ya punda nchini Somalia yatachukuliwa kama ‘shughuli za al-shabab’ kufuatia taarifa kuwa wapiganaji hao wanatumia punda kusafirishia silaha.Meja Emmanuel Chirchir ametumia Twitter kuwaonya Wakenya kutowauza punda wao kwa wapiganaji hao.
Majeshi ya Kenya yako Somalia kutengeneza mpaka wa kivita baada ya kuwatuhumu al-Shabab kuhusika na matukio ya utekaji nyara.
Al-Shabab, linalodhibiti Somalia kusini limekanusha tuhuma hizo.
Linaituhumu Kenya kwa kupanga uvamizi kamili nchini Somalia.
Jumanne Meja Chirchir kupitia mtandao Twitter alionya kuwa kambi za al-shabab karibu na miji 10 ya Somalia zitashambuliwa wakati wowote na kuwataka wakazi wake kuondoka.
Hata hivyo, hakuna mashambulizi yoyote ambayo ameshatokea mpaka sasa.
Picha za video ambazo ametuma akisema ni boti ndogo ya al-shabab ikizama na kuua wapiganaji 18. Ameonya kuwa hakuna ndege yoyote inayoruhusiwa kutua katika mji wa Baidoa unaodhibitiwa na al-Shabab kufuatia taarifa kuwa al-shabab wanaingiza silaha kwa ndege katika mji huo.
Katika taarifa mpya kupitia Twitter msemaji wa jeshi la Kenya alisema bei ya punda imepanda kutoka $150 (£100) mpaka $200 kufuatia kuongezeka kwa mahitaji punda kwa al-shabab.
"Makundi yoyote ya punda yanayotembea na mizigo yatachukuliwa kuwa ni shughuli za al-shabab," ameandika.
"Kuuza punda kwa al-Shabab kutaathiri harakati zetu nchini Somalia," inafafanua.
Mwandishi wa BBC Afrika Mashariki Will Ross anasema haijafahamika wazi iwapo al-Shabab wanatumia punda kwa sababu barabara zina matope na hazitpitiki kwa magari au wanaogopa kuonekana kupitia ndege za kivita.
Meja Chirchir pia alisema, ndege yoyote "inayoruka katika anga la eneo hilo," itachukuliwa kuwa ni tishio.
"Ndege yoyote isitue mjini BAIDOA. Mtu yeyote atakayevunja amri hii atakuwa amejiingiza mwenyewe kwenye hatari," aliandika.
Al-Shabab, ambalo lina uhusiano na al-Qaeda, limejikuta kwenye vita na serikali ya mpito inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kwa kudhibiti sehemu ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment