Monday, November 7, 2011

Lema akubali kutoka rumande

 SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kutua jijini Arusha na kumtembelea gerezani Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, na kumwomba atoke ili aweze kuhudhuria vikao vya Bunge, hatimaye uamuzi huo umeridhiwa kwa mbunge huyo kuachiwa leo.

Hata hivyo, kama Lema alivyoweka sharti la kutaka polisi wamruhusu kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara mara baada ya kuachiwa, tayari jeshi hilo limesalimu amri na kuruhusu mkutano huo utakaotanguliwa na mapokezi ya mbunge huyo.

Lema alifikia uamuzi wa kwenda mahabusu ya gereza la Kisongo baada ya kukataa dhamana, akipinga uonevu na manyanyaso ya polisi wilaya ya Arusha wakiongozwa na OCD, Zuberi Mwombeji.
Maamuzi yake ya kwenda mahabusu, yameonekana kuleta mtafaruku mkubwa jijini hapa baina ya polisi na wananchi, kiasi cha amani kutoweka kutokana na wafuasi wake wengi kuendesha migomo wakidai jeshi hilo linamwonea.

Ni katika vuta nikuvute hiyo, jeshi hilo limemwangukia Lema, kwa kuwatuma makamishna wakuu juzi ili kumwomba akubali kutoka rumade kwa kile kilichodaiwa ‘kurejesha hali ya amani na utulivu jijini humo’.
Leo viunga vya Jiji la Arusha vinatarajiwa kulindima kwa shangwe na vifijo ambapo CHADEMA wakiwa na mbunge wao Lema, watafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya NMC, eneo la Unga Ltd, utakaohutubiwa na viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willbrod Slaa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, jana aliliambia Tanzania Daima kwa njia ya simu kwamba jeshi hilo tayari limeruhusu mkutano huo utakaotanguliwa na mapokezi makubwa ya Lema akitokea rumande.
“Tumetoa kibali kwa CHADEMA kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya NMC, kuanzia saa 8:00 mchana. Nasisitiza kuwa tulichoruhusu ni mkutano wa hadhara na siyo vinginevyo,” alisema Kaimu Kamanda Mpwapwa.

Kwa mujibu wa Katibu wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, maandalizi ya mkutano huo utakaohudhuriwa na viongozi wengine wa kitaifa wakiwemo wabunge Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Hayness Kiwia (Ilemela), tayari yamekamilika huku magari mawili aina ya Fusso maalumu kwa mawasiliano ya umma yakiwa yamewasili tangu jana.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Arusha, Ephatah Nanyaro, ambaye wilaya yake ndiyo mwenyeji wa shughuli hiyo, aliwataka wananchi na wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kusikiliza ujumbe maalumu utakaotolewa na viongozi wa chama hicho kuhusu migogoro na vurugu za mara kwa mara kati ya polisi, viongozi, wanachama na wapenzi wa chama hicho.

Nanyaro alisema kabla mkutano kuanzia saa 7:00 kutakuwa na shamra shamra za kumpokea Lema anayetajiwa kutoka nje kwa dhamana leo baada ya kuamriwa na chama chake kufanya hivyo.
Agosti 11, mwaka huu, CHADEMA ilifanya mkutano mjini hapa na kueleza sababu za kuwatimua waliokuwa madiwani wake walioingia muafaka na wenzao wa CCM bila kibali cha chama taifa ambapo Mbowe na Dk. Slaa waliipa Serikali siku 30 kutatua mgogoro wa umeya la sivyo wangeamua kwenda kuweka kambi ofisi za manispaa hadi ufumbuzi utakapopatikana.

Pamoja na Lema kuzungumza na wananchi, mkutano huo pia utatumiwa na viongozi hao kutoa msimamo kuhusu viongozi wake kuandamwa na vyombo vya dola huku wengi wakifunguliwa kesi mbalimbali mahakamani.

No comments:

Post a Comment