Kutokana na mashitaka hayo, Mbowe ameunganishwa na washtakiwa wengine 27 wanachama wa chama hicho, waliofikishwa mahakamani hapo Jumanne iliyopita wakikabiliwa na mashtaka kama hayo, akiwemo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu .
Mbowe ambaye pia Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni, ameunganishwa kwenye kesi hiyo ya jinai namba 454/2011 ambapo watuhumiwa wote kwa kwa pamoja, wanadaiwa kufanya kusanyiko isivyo halali katika viwanja vya NMC, eneo la Unga Ltd, Manispaa ya Arusha Novemba 7 mwaka huu.
Hata hivyo Mbowe ambaye anakuwa mshitakiwa wa 28 kwenye kesi hiyo, alikana mashitaka yote mawili yaliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Haruna Matagane akisaidiwa na mwenzake, Agustino Kombe.
Upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili Method Kimomogoro na Issa Rajabu, uliiomba mahakama hiyo kumpa dhamana mteja wao kwa masharti sawa na wenzake.
Hakimu Devotha Kamuzora anayesikiliza kesi hiyo, alikubaliana na maombi hayo na kumpa dhamana Mbowe, kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho na barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ambao walitia saini hati ya dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja.
Mwenyekiti huyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti . Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu itakapotajwa.
Maelezo ya wakili
Katika maelezo ya hati ya mashitaka, Wakili Matagane alidai washitakiwa wote kwa pamoja walikusanyika isivyo halali kwenye viwanja vya NMC usiku wa Novemba 7 hadi Novemba 8 mwaka huu saa 12.00 asubuhi kwa lengo la kutenda kosa wakati shtaka la pili, ni kukataa kutii amri halalii ya polisi iliyotolewa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Peter Mvulla, kuwataka watawanyike.
Mbowe aliyejisalimisha mwenyewe polisi saa 5:45 juzi baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Kaimu Kamanda wa Polisi, Akili Mpwapwa, alifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi akiwa ndani ya gari namba PT 1844 aina ya Toyota Land Cruiser, lililosindikizwa na gari jingine lililojaa askari waliovalia sare za jeshi hilo huku wakiwa wakiwa wamebeba silaha.
Mwenyekiti huyo aliyefika eneo la viwanja vya Mahakama Saa 3:45 asubuhi, aliongozwa moja kwa moja kwenye chumba maalumu cha kusubiria kabla ya kufikishwa mbele ya hakimu kusomewa mashtaka yake saa 4:00 huku umati mkubwa wa wafuasi wa Chadema ukiwa umefurika ndani na nje ya mahakama hiyo.
Kauli ya Pinda kuhusu Chadema
Wakati hayo yakiendelea Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoboa siri kuhusu maandamano ya mara kwa mara yanayofanywa na Chadema kwa kutamka kwamba yanaiumiza kichwa serikali.
Akijibu maswali papo kwa papo bungeni jana, Pinda alisema ; "Staili yenu hiyo (Chadema) ya maandamano, inatupa shida sana, tunapata taabu kila wakati kufikiria maandamano badala ya mambo ya msingi.”
Waziri mkuu alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliyetaka kujua, pamoja na mambo mengine dhamira na msimamo wa serikali ya kutatua mgogoro wa umeya wa Arusha.
Mnyika alisema tatizo kubwa la mgogoro wa Arusha ni uchaguzi wa meya ambao Chadema imeonyesha dhamira ya dhati kutafuta suluhu hivyo, akataka msimamo Pinda kwa maelezo kuwa mgogoro huo umesambaa nchi nzima na kama haiwezekani kupatikana suluhu Chadema watajua cha kuwaeleza wanachama wao.
Katika jibu lake Pinda aliitaka Chadema kutokuza jambo hilo kwa namna Inavyolichukulia ,“Tusikuze sana mambo kwamba mgogoro huo sasa umesambaa, wapi Mnyika? Wapi? Kwa staili yenu (Chadema) ya maandamano kila mahali, sisi serikalini tuna mengi ya kufanya, hatuwezi kila siku tuwe tunashughulikia matatizo yenu tu. 'People's Power' kila kukicha, haileti suluhu ya matatizo yenu, mnahitaji kubadilika,” alisema Pinda
Alisema wakati mwingine serikali inaacha kufikiria mambo ya maendeleo kwa wananchi na kujikuta inafikiria maandamano ambayo yamekuwa yakishinikizwa mara kwa mara na Chadema nchi nzima.
Pinda alisema staili hiyo ya Chadema kufanya maandamano kwa kile inachoiita, kutegemea nguvu ya umma, imekuwa ikimuuza zaidi yeye binafasi, "kwa kweli mimi naumizwa na hili".
Aliongeza kwamba, maandamano hayo wakati mwingine yanaonyesha namna chama hicho kisivyo na dhamira ya kweli katika kupata suluhu ya matatizo mbalimbali ikiwemo ya mgogoro wa umeya wa Jiji la Arusha.
“ Staili yenu ya 'People's Power, People's Power !' kila kukicha, inatunyima usingizi. Tunashindwa kufanya shughuli nyingine kwa sababu ya kuifikiria Chadema,” alisema Pinda.
Alisema katika suala la Arusha, imeonekana ni jambo la kisiasa ambalo alimweleza Msajili wa Vyama awasiliane na pande zote mbili ikiwemo CCM ili kuona namna ya kukaa meza moja na kulimaliza .
Awali, Waziri Mkuu akijibu swali kama hilo kutoka kwa Mbunge wa Korogwe, Stephen Ngonyani, aliitaka Chadema kujitathmini ili kuona kama kweli kinahitaji suluhu katika mgogoro wa Arusha badala ya kuilaumu serikali.
Katika swali lake la msingi, Ngonyani alionesha wasiwasi wake kwamba mgogoro wa umeya wa Arusha hivi sasa unatishia hata biashara ya utalii katika jiji hilo na kutaka Mbunge wa Arusha Lema apewe dhamana kama njia ya kupunguza mvutano.
"Mheshimiwa Waziri Mkuu, siku hizi kila kukicha ni vurugu na migogoro Arusha. Sasa hivi Arusha utalii hakuna na biashara hazifanyiki. Kwa nini serikali inazuia dhamana ya Lema?”
Akijibu swali hilo, mbali na kukiri kwamba migogoro jijini Arusha inaathiri sekta ya biashara na utalii, Waziri Mkuu Pinda, alikanusha fikra kwamba serikali inahusika kwa namna yoyote katika kupalilia vurugu hizo, ikiwamo kuzuia dhamana ya mbunge huyo wa Arusha Mjini.
“Ni kweli Arusha kuna migogoro mingi lakini, bado ni tulivu. Ila kama Watanzania, lazima tuzingatie unalolisema. Sio kweli kwamba serikali inazuia dhamana ya Mheshimiwa Lema. Vurugu zote hizo, mara nyingi zinazaa kesi,” alisema Pinda na kuendelea;
“Tarehe Oktoba 28, 2011 Lema na wenzake kadhaa walikamatwa, wakafikishwa mahakamani na kupewa dhamana hadi Oktoba 31, 2011 walipotakiwa kufika tena mahakamani. Kimsingi mashtaka yale yote, yanastahili dhamana na mahakama ilikubali watuhumiwa wote wadhaminiwe.”
“Kilichotokea kwa Lema kwa sababu ambazo mimi sizijui, alikataa dhamana, akisema anataka kubaki gerezani. Wenzake walidhaminiwa na Lema alipelekwa gerezani kama alivyotaka hadi Novemba 14.”
“Ilipofika Novemba 7 (2011), Chadema walikubaliana na mawakili wao kupeleka maombi maalumu mahakamani ili wakamtoe Lema. lakini hakimu akawaambia kesi tumeiahirisha hadi Novemba 14. Sasa hii ni Mamlaka ya Mahakama sio serikali. Tutegemee tu kwamba siku hiyo yanaweza kutoka maamuzi ya kumtoa Lema garezani.”
Pinda alisema kwa mazingira yalivyo, hayuko tayari kutoa maagizo mapya juu ya mgogoro wa Arusha kwa kuwa haoni nia ya dhati ya Chadema kutaka suluhu.
Maandamano Dar
Jijini Dar es Salaam, maandamano yaliyopangwa kufanywa na Baraza la Vijana la Chama hicho (Bavicha) Mkoa, kupinga kile walichokiita kukamatwa na kunyanyaswa kwa viongozi wao wa kitaifa, yamesitishwa.
Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alitangaza kusitishwa maandamano hayo baada ya kuwasili eneo lililopangwa kufanyika maandamano hayo.
Katika utekelezaji wa kusitisha maandamano hayo, viongozi wengine wa chama hicho waliwasili eneo hilo na nakulazimika kuwaomba wafuasi wa chama hicho kutawanyika kutokana na kwamba mpango huo umesitishwa.
Mnamo saa 3:00 asubuhi, umati mkubwa wa wafuasi wa chama hicho ulitanda eneo la Kimara Kona pamoja na Ubungo, yalipopangwa kuanzia maandamano hayo.
Akizungumzia kusitishwa kwa maandamano hayo, Heche alisema wamefikia uamuzi huo baada viongozi wakuu wa chama hicho kufanya majadiliano na maofisa wa Jeshi la
Polisi kuhusu madai ya kero zao.
“Tumepata maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wetu Mbowe na Katibu Mkuu Dk Slaa ya kwamba tusitishe maandamano kwa sababu kuna majadiliano yanaendelea kati yao na maofisa wa Jeshi la Polisi,” alisema Heche.
Aliongeza kuwa kama hakutakuwa na muafaka katika majadiliano hayo, wataingia tena mtaani na kuandamana mpaka kero zao zitakapopatiwa ufumbuzi.
Hali ya ulinzi
Hata hivyo, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam huku kamatakamata ikiwakumba baadhi ya wafuasi wa chama hicho waliovalia mavazi ya chama hicho.
Saa 5: 10 katika eneo la Ubungo gari la polisi lenye namba PT 1818 ambalo lilikuwa limebeba askari waliokuwa na silaha za moto, walikuwa wakiwatangazia wananchi waliokuwa wamekaa katika makundi kutawanyika .
Watu saba waliokuwa wamevalia mavazi ya chama hicho walikamatwa na kufikishwa katika kituo kidogo cha Polisi Urafiki, huku wengine wakiwa wamekamatwa na kubebwa kwenye magari ya polisi ambayo yalikuwa yakizunguka mitaani .
Baadhi ya viongozi wa chadema, walifika katika kituo cha polisi urafiki ambako wafuasi hao saba waliokuwa wamewekwa rumande kwa muda wa saa mbili.
Viongozi hao walifanikiwa kuwatoa kwa dhamana na walitakiwa kubadilisha mavazi hayo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Suleimani Kova alisema hali ya usalama katika jiji la Dar es Salaam ni shwari na hakuna tukio lolote la uvunjivu amani ambalo limejitokeza.
“Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kwamba hakuna tukio lolote la uvunjifu amani ambalo limejitokeza “ alisema Kova.
Kova alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha linaimarisha ulinzi katika maeneo yote ya jiji.
No comments:
Post a Comment