MILIO ya risasi za moto na mabomu ya machozi jana vililifanya Jiji la Mwanza kuchafuka na baadhi ya barabara kufungwa na shughuli za kijamii kusimama kwa zaidi ya saa mbili, kutokana na kuzuka kwa vurugu kubwa na mapambano baina ya waumini wa dini ya Kiislamu na Jeshi la Polisi mkoani hapa.
Magari ya abiria na hasa daladala, zilikatisha safari zake na magari madogo yalilazimika kuegeshwa maeneo ya mbali kutokana na vurugu hizo, huku wananchi wakihaha huku na kule kuokoa maisha na mali zao. Baadhi ya wananchi walijeruhiwa na mabomu hayo akiwamo mwanamke anayeuza magazeti katika eneo la Bantu, aliyejeruhiwa shingoni na katika mikono yake.
Baadhi ya wafanyakazi waliokosa usafiri walilazimika kukatiza njia za vichochoroni ili kufika mjini umbali wa kilometa tano kutoka eneo la Bantu iliko mahakama hiyo.
Vurugu hizo kubwa zilizoanza jana majira ya asubuhi, zilitokana na waumini hao wanaodai kuchukizwa na hatua ya kupewa dhamana kwa watu wanne wanaoshitakiwa kwa kosa la kuchoma kitabu kitakatifu cha Kurani kuizingira Mahakama ya Mwanzo iliyoko eneo la Bantu kwa lengo la kuwakamata na kuwaadhibu kwa mujibu wa sheria za dini ya Kiislamu.
Wakiwa wametanda nje ya mahakama hiyo, waumini hao wa Kiislamu, walisikika wakilalamika, wakihamasishana kuchukua hatua hiyo kwa madai kwamba hawaridhishwi na hatua ya kuahirishwa kila wakati kwa kesi na zaidi kudhaminiwa kwa wahusika.
’’Tutatoa hukumu yetu hapa. Hatutaki kesi hii iendelee kuahirishwa mara kwa mara, tunataka haki itendeke, vinginevyo tutawahukumu hapahapa, maana walichana Kurani tukufu,” alisikika muumini mmoja wa Kiislamu akisema nje ya mahakama hiyo.
Polisi walifika haraka baada ya kupata taarifa za tishio hilo na kuwataka waumini hao kutawanyika na kuondoka katika eneo hilo, jambo ambalo lilikataliwa na umati huo wa watu. Kama watu waliojua kitakachotokea, waumini hao walianza kujikusanya na kuanza kuwarushia mawe polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alisema polisi walilazimika kutumia nguvu hiyo kubwa kwa lengo la kuimarisha usalama wa raia na mali zao, ikiwa ni pamoja na kuwatawanya waumini hao wa Kiislamu wasiendelee kufanya fujo mahakamani hapo.
Alisema tayari watu 19 wakiwamo baadhi ya viongozi wa Kiislamu wamekamatwa na wanafanyiwa mahojiano maalumu na kwamba jeshi hilo linawasaka watu wengine wanaodaiwa kusababisha vurugu hizo kubwa.
"Polisi hatuwezi hata siku moja kuruhusu uvunjifu wa amani utokee mahala popote.
Na ndiyo maana tumelazimika kutumia nguvu kwa ajili ya kurejesha usalama. Kuna watu 19 tumewakamata, na wamo baadhi ya viongozi wao...sheria lazima ifuate mkondo wake katika hili,” alisema Kamanda Barlow.
Hivi karibuni waumini wa dini ya Kikristu walifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo jijini Mwanza wakituhumiwa kuchoma Kurani tukufu, baada ya mwanamke mmoja muumini wa dini ya Kiislamu kuombewa na kubahatika kupata mtoto katika kanisa moja jijini hapa na waumini hao kuamua kuchoma moto Kurani hiyo kinyume cha sheria za nchi. |
No comments:
Post a Comment