KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wafuasi wa chama hicho 27 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Arumeru kujibu mashitaka matatu.
Viongozi hao na wafuasi wao walifikishwa mahakamani hapo jana mchana wakiwa kwenye karandinga na kuwekwa mahabusu kwa muda wakisubiri kusomewa mashitaka ya kufanya mkusanyiko usio halali saa 11 alfajiri juzi na jana eneo la NMC.
Wanashitakiwa pia kwa kukaidi amri ya Polisi ya kutawanyika na katika mashitaka yanayomhusu Dk Slaa peke yake anadaiwa kutoa matamshi ya uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, Zuberi Mwombeji.
Akiwasomea mashitaka Wakili wa Serikali Hamisi Mategane, alisema washitakiwa kwa pamoja walifanya makosa hayo na kukaidi amri ya Polisi lakini washitakiwa hao walikana mashitaka. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 22 na washitakiwa 18 walipata dhamana na wengine kurudishwa mahabusu.
Jana asubuhi jijini hapa hali ilikuwa tete baada ya polisi kuwasambaratisha kwa mabomu ya machozi wafuasi wa Chadema. Mabomu hayo yalianza kurindima saa 10 hadi 11 alfajiri na kusababisha tafrani kubwa katika maeneo ya Jiji.
Watu walioshuhudia tukio hilo, walisema hawajapata kuona mabomu yakirindima kwa muda mrefu kiasi hicho. Walisema viongozi, wafuasi na wanachama wa Chadema waliofurika katika uwanja wa NMC kwa ajili ya mkesha waliouita kuwa ni wa ukombozi, walitawanyika kila mmoja kivyake.
Baadhi ya viongozi waliokuwa katika mkesha huo ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki na viongozi wa chama hicho Arusha.
Chadema walitangaza juzi kuanza kwa mkesha huo wakipinga hatua ya Mahakama kumnyima Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, dhamana. Lema na wenzake wanakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya maandamano na mkusanyiko wa usio halali, tukio linalodaiwa kutokea baada ya kumaliza kusikiliza kesi nyingine inayomkabili ya kupinga matokeo yake ya uchaguzi.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Kaimu Kamanda wa Polisi, Akili Mpwapwa, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari, akithibitisha kukamatwa kwa watu 20 wakiwamo, Dk. Slaa (63) na Lisu (43).
Wengine waliokamatwa ni David Godfrey (18), Ally Hussein (20), Frank Chami (24), Stella Mushi (21), Francis Samweli (20), Paulo Meena (18), Beatrice John (28), Matei Thobias (38), Davies Sedeka (29) na Wilson Andrea (24).
Wengine ni Wichad Urasa (27), Abubakar Mrema (25), Peter Davis (14), Poloches Blamo (36), John Masaki (53), Stephano Swai (33), Mohamed Mhoji (21), Titus Ullo (30), Nelson Kimaro (23), Meshack Beture (23) na Jimmy Evarist (22) wote wakazi wa Arusha.
Alisema kilichotokea na kusababisha kukamatwa kwao ni Chadema kuomba kibali Novemba 4 kufanya mkutano kwa siku saba mfululizo, na kupitia barua yao namba CDM/MKA/PL.11/014 iliyosainiwa na Katibu wa Chama hicho wa Mkoa wa Arusha, Amani Golungwa na nakala kwa viongozi wa Taifa wa chama na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Arusha.
Alisema barua hiyo ilipelekwa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, Zuberi, ambaye kupitia vikao vyao walitoa kibali juzi kwa barua namba AR/A.24/29/VOL.VII/26 kuwakubalia kufanya mkutano NMC.
Alisema pamoja na kibali hicho polisi walitoa masharti kuwa ufanyike kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12.30 jioni na kusiwe na lugha za uchochezi, kashfa na matusi dhidi ya vyama vingine vya siasa na viongozi wao. Masharti mengine walitakiwa wasikashifu dini zingine au madhehebu, wahakikishe wanazingatia muda wa kuanza na kumaliza, kusiwe na maandamano ya watu, magari, pikipiki wala baiskeli.
Hata hivyo, Chadema walifanya mkutano huo na kutoa lugha za uchochezi, wakitaka watu wakeshe NMC ili kuomboleza mpaka Lema atoke. Mpwapwa alisema walimkamata Dk. Slaa, akiwa amejificha katika gari akiwa na bastola namba T2-CAR-61074-327963 aina ya Walther, yenye risasi saba.
Pia mshitakiwa Daniel Mgogo, ambaye ni mkulima, alikutwa na bastola namba H-447577 -CAT- 5802 aina ya Bereta yenye risasi 10. “Tunazifanyia uchunguzi kubaini kama wanazimiliki kihalali au la na nia yao ya kwenda nazo katika mkutano ilikuwa nini, ila kwa sasa tumefungua tu mashitaka ya mkusanyiko bila kibali na lugha za uchochezi,” alisema Mpwapwa.
Pia Jeshi hilo lilimwomba Mbowe ajisalimishe Polisi kwa sababu naye ni miongoni mwa washitakiwa, kwani alikimbia baada ya wenzake kukamatwa.
No comments:
Post a Comment