Thursday, November 3, 2011
WAFUASI CHADEMA WAZUIWA KUMWONA LEMA GEREZANI, RISASI, MABOMU VYARINDIMA MWANZA
VURUGU kubwa zimetokea jana katika majiji ya Arusha na Mwanza kiasi cha kuwalazimu polisi kutumia mabiomu ya machozi na baadhi ya watu kutiwa nguvuni.Jana asubuhi jijini Arusha, watumishi wa daladala zinazojulikana huko kama vifodi, waliitisha mgomo kulaani kile walichokiita unyanyasaji wa polisi hatua iliyowalazimu askari hao kuingilia kati na kuwatia mbaroni zaidi ya watu 30.
Mgomo huo ulianza majira ya saa mbili asubuhi na kudumu hadi saa 5:00 asubuhi.
Pia polisi na askari wa Magereza walikuwa na kibarua kizito kuwadhibiti wafuasi wa Chadema kwenda katika Gereza la Kisongo kumwona Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Polisi waliweka ulinzi mkali wakiwazuia na kuwahoji watu wote waliokuwa wakielekea njia ya Kisongo liliko Gereza hilo Kuu la Mkoa wa Arusha ambako Lema yuko mahabusu.
Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wanataka kwenda kumwona mbunge huyo katika utaratibu wa kawaida wa kuwaona wafungwa na mahabusu katika gereza hilo siku za Jumatano, Jumamosi na Jumapili.
Baadhi ya wananchi waliofanikiwa kupenya kupitia njia za vichochoroni na kufika gerezani hapo, walikumbana na kizingiti kingine cha askari Magereza ambao waliwazuia kumwona mbunge huyo kwa madai idadi ya watu inayotakiwa kumwona ilishatimia.
Ofisa Magereza mwenye cheo cha mkaguzi msaidizi, aliyekuwa amevaa beji yenye jina la J. Mmari alizungumza na wananchi hao kwa niaba ya mkuu wa gereza hilo akisema sheria inaelekeza kuwa siku ya Jumatano wanaoruhusiwa kumtembelea mtuhumiwa ni mawakili wake na wageni wasiozidi watatu, lakini kwa busara uongozi wa gereza uliamua kuruhusu watu zaidi.
“Mpaka sasa walioingia kumwona Lema wamezidi na hatuwezi kuendelea kuruhusu kwani tangu saa 2:00 asubuhi Mheshimiwa ametembelewa na idadi kubwa na anaongea nao kwa zaidi ya dakika kila kundi. Tafadhalini wengine njooni Jumamosi na Jumapili,” alisema Mmari.
Kauli hiyo iliamsha jazba na hasira za vijana walioanza kutoa maneno makali na kumlazimu mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Arumeru, Joshua Nassari kuwatuliza.
Mgomo wa daladala
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alisema hatua ya kuwakamata watu katika mgomo huo wa daladala kwa nyakati na sehemu tofauti ilikuja baada ya polisi kupata waraka ulioandikwa na watu wasiojulikana kutangaza na kuhamasisha mgomo huo uliokuwa na malengo makuu matatu, ikiwamo kile kilichoelezwa kuwa kupinga ni kulaani kauli ya OCD kuwaita wananchi mapanya.
Katika mgomo huo, makundi ya vijana wa daladala walikuwa wakiwashambulia wenzao waliokaidi kushiriki kwa kuendelea na kazi ya kusafirisha abiria, pia ulilenga kulaani na kupinga kile kilichoelezwa kuwa ni udhalilishaji na ukatili wa jeshi la polisi.
Washiriki wa mgomo huo pia walikusudia kufikisha ujumbe kwa watendaji serikalini kuacha kile walichoeleza kuwa ukibaraka, udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya raia. Hadi jana jioni, viongozi mbalimbali walikuwa wakiendelea na harakati za kuhakikisha mgomo huo unadhibitiwa.
Kamanda Mpwapwa akionyesha nakala ya waraka huo aliodai aliupata kwa njia za kiintelijensia alisema alifanikiwa kudhibiti mgomo huo, huku baadhi ya vijana waliohisiwa kuhusika kuuandaa akiwamo kada maarufu wa Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho, Kata ya Kati, Rashid Shubeti
wakizuiwa na polisi kutoka majumbani mwao.
Shubeti tayari alishatoa taarifa kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa, Leonard Paul kuhusiana na kuvamiwa nyumbani kwake na watu wenye silaha waliojitambulisha kuwa polisi waliomtishia kumpiga risasi iwapo angethubutu kutoka nyumbani kwake.
Polisi yachunguza
Katika hatua nyingine, Polisi Mkoa wa Arusha imefungua jalada ya uchunguzi dhidi ya kauli ya kuwaita panya wananchi na wanachama wa Chadema inayodaiwa kutolewa na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Zuberi Mwombeji.
Kamanda Mpwapwa alisema sambamba na uchunguzi huo, jalada hilo pia litahusika na uchunguzi wa makosa yanayodaiwa kutendwa na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na watu wengine 18 waliofikishwa mahakamani Jumatatu iliyopita.
“Kwa sababu mambo yote mawili ya uhalifu unaodaiwa kutendwa na Lema na wenzake pamoja na madai ya OCD kuwaita wananchi mapanya yalitokea sehemu moja na siku hiyohiyo, tutayachunguza kwa pamoja kubaini ukweli na kupata ushahidi ili haki itendeke kwa wote,” alisema Kamanda Mpwapwa.
Oktoba 28, mwaka huu akiwa eneo la Mahakama Kuu Kanda ya Arusha alikokuwa akikiliza kesi ya kupinga ubunge wa Lema iliyofunguliwa na wapiga kura watatu, OCD Mwombeji anadaiwa kuwaita wananchi wanaoaminika kuwa wafuasi wa Chadema mapanya.
Akizungumzia madai hayo jana kwa njia ya simu, OCD Mwombeji alikana kutoa kauli hiyo na kusema hizo ni propaganda zinazoenezwa kuhalalisha uhalifu au kutafuta huruma ya umma kwa makosa yaliyotendeka.
“Sijawahi wala siwezi kumwita mwanadamu mwenzangu panya. Ukiachilia mbali maadili na malezi mema niliyopata kutoka kwa familia yangu, hata wadhifa na cheo changu hakinipi uhalali wa kutoa kauli kama hiyo, ninaomba umma wa Arusha usubiri uchunguzi unaoendelea kwani ukweli utadhihiri,” alisema OCD Mwombeji.
Vurugu za Mwanza
Jijini Mwanza, mabomu ya machozi yalitumika katika Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mwanza baada ya waumini wa Kiislamu kugoma kutoka nje ya eneo hilo kupisha shughuli za mahakama kuendelea baada ya kuahirishwa kwa kesi namba 233/2011 inayowakabili washtakiwa wanne, Mchungaji Tumaini Jumanne, Dickson Maghai, Petro Mashauri na Karista Mrom.
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka kufanya mkusanyiko usio halali na kuingia ndani ya nyumba ya Husna Hamisi (40) bila idhini yake na kutenda kosa la kuishambulia na kuikashifu dini ya Kiislamu hivyo kuchochea hasira kwa waumini wa dini hiyo na kusababisha uvunjifu wa amani.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 21, mwaka huu katika Mitaa ya Lumala wakati wakiwa katika maombi ya kumuombea Husna akiwa mgonjwa ambaye ni Muislamu.
Vurugu za jana zilizotokana na kuahirishwa kwa kesi hiyo, zilisababisha maduka, benki na ofisi mbalimbali jijini humo kufungwa huku watu wakikimbizana kujificha wakihofia vurugu hizo zilizosambaa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza.
Patashika hiyo ilianza saa 3: 22 asubuhi hadi saa 5: 35 na muda wote huo, maduka na huduma mbalimbali zilisimama katika maeneo husika baada ya Hakimu Janeth Masese kuahirisha kesi hiyo alipomaliza kusikiliza maelezo ya awali ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Lameck Merunde aliyeomba kesi hiyo kupangiwa siku nyingine ya kusikilizwa. Hakimu Merunde alipangia kesi hiyo kusikilizwa tena Novemba 24, mwaka huu.
Baada ya hatua hiyo, viongozi wa Kiislamu waliokuwa ndani wakisikiliza kesi hiyo kutoka nje ya viwanja vya mahakama ambako kulikuwa na kundi kubwa la waumini na kuwaeleza hali iliyotokea katika shauri hilo lakini walionyesha kutokubaliana na hatua hiyo na kuanza kupaza sauti za Takbiir’.
Hatua hiyo ya iliwafanya maofisa wa polisi waliokuwapo mahakamani hapo kuanza kuzunguka maeneo hayo ya mahakama kisha kuwataka wote waliokuwa jirani na eneo hilo kuondoka ili watuhumiwa wengine watolewe nje ya mahakama. Waligoma wakitaka watolewe wakiwaona hivyo kuzusha mvutano baina yao na polisi.
Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza (RCO), Deusdedit Nsimeki alijaribu kuzungumza na waumini hao akiwataka watii na kuondoka eneo hilo lakini jitihada zake hazikuzaa matunda.
Baada ya hatua hiyo polisi waliamua kutumia nguvu kuwatawanya na kisha kuwafuatilia waumini hao katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza ambako mabomu ya machozi yalitumika katika baadhi ya maeneo hivyo kusimamisha shughuli mbalimbali zikiwamo maduka, benki na ofisi.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo alisema: “Mahakama inao uhuru wake katika uendeshaji wa kesi, lakini walichokuwa wanatakiwa kufanya wenzetu Waislamu ni kuiachia ifanye kazi yake kama nilivyokubaliana nao wiki chache zilizopita pale tulipokutana katika hafla ndogo ya chakula na viongozi wa dini.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow alisema watu 19 wamekamatwa na mmoja amejeruhiwa kutokana na vurugu hizo.
Habari hii imeandaliwa na Peter Saramba na Mussa Juma, Arusha na Frederick Katulanda na Sheilla Sezzy, Mwanza
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment