Maafisa wanasema watu wasiopungua wawili wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine 11 kujeruhiwa baada ya watu waliokuwa na silaha kushambulia kanisa moja usiku kaskazini mwa Nigeria.
Mashambulio hayo yametokea katika mji wa Zonkwa ulio katika jimbo la Kaduna ambao awali ulikabiliwa na ghasia kubwa wakati wa uchaguzi wa Aprili.Jimbo la Kaduna limegawanyika kwa misingi ya kisiasa,kidini na kikabila.
Maelfu ya waislamu wa kabila la Hausa na Fulani walifurushwa kutoka makwao mwezi Aprili.
Mwandishi wetu anasema kuwa baadhi ya wale walioshambuliwa waliahidi kulipiza kisasi ikiwa nipamoja na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Boko Haram ambalo makao yake yako katika jimbo la kaskazini la Borno.
Anasema kuwa watu 3,000 bado wanaishi kambini katika mji mkuu wa jimbo hilo la Kaduna baada ya nyumba zao kuteketezwa Zonkwa katika ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu ambazo zilisababisha vifo vya watu kadhaa.
Msemaji wa polisi amemwambia mwandishi wetu kuwa baadhi ya waliopigwa risasi katika mashambulio haya ya sasa ambayo yaliwalengwa waumini waliokuwa katika mkesha wa kidini wako katika hali mahtuti.
Nigeria imegawanyika mara mbili ambapo upande wa kaskazini una Waislamu wengi na upande wa kusini Wakristo ndio wengi.
Katika uchaguzi wa mwezi Aprili Patrick Ibrahim Yokowa aliibuka mshindi na kuwa gavana wa kwanza wa Kiksrito katika eneo hilo.
Yeye ni mwanachama wa People's Democratic Party, ambacho ndicho kinachotawala katika kiwango cha kitaifa.
Chama cha upinzani cha CPC wafuasi wake wengi wanatoka katika makundi ya kiislamu.
Zaidi ya watu 1,000 wameuawa katika miaka ya hivi karibuni katika Jimbo jirani la Plateau katika msururu wa mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya makundi yanayohasimiana kwa misingi ya kikabila,kidini na kisiasa.
No comments:
Post a Comment