Thursday, November 3, 2011

Muswada wa katiba urudishwe kwa wananchi kwanza-Wanaharakati

Na Rehema Maigala

WANAHARAKATI wa Baraza la Katiba Tanzania wamesema muswada utakaowasilishwa bungeni usomwe kwa mara ya kwanza ili kuwapa fursa mwananchi kutoa maoni yao kama katiba ya sasa inavyoelekeza.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa jukwaa la Katiba Tanzania Bw. Deus Kibamba, alisema iwapo muswada huo utasomwa kwa mara ya pili na tatu utakuwa ni upotoshaji kwa kuwa wananchi hawatakuwa na fursa ya kutoa maoni yao.

"Muswada huu ni mpya hivyo inatakiwa itambulike kuwa ndio unasomwa kwa mara ya kwanza, ule uliosomwa bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Aprili haukuleta mafanikio na kwa sasa hauwezi kuletwa kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya pili kana kwamba ulisomwa kwa mafanikio,"alisema Bw. Kibamba. 

Alisema kukataliwa kwa muswada huo kwa mara ya kwanza ni dhahiri kuwa yapo  baadhi ya mambo ambayo yameweza kubadilika kulingana na maoni ya wasomi, wataalam na wananchi juu ya muswada huo.

Hata hivyo alisema imeoneka kuwa kuna kusuasua katika kukamilisha muswada huo kwa ajili ya kuwasilisha bungeni na kwamba ulitakiwa kuwasilishwa mpya katika mkutano wa bajeti uliokamilika mwezi Agosti mwaka huu.

Alisema katika awamu hii muswada huo umeshereweshwa kuchapishwa katika gazeti la serikali na kunyima fursa wananchi kuuona, kuuchambua na kuujadili kabla ya kwenda bungeni.

Alisema katika mikutano yao ya pamoja na makongamano na semina na wananchi, walipendekeza kuwa muswada mpya ujadiliwe katika kila mkoa kuwe na kituo cha kujadili huo muswada.

Alitaja vipengele ambavyo vinaonyesha serikali kukosa umakini katika kuandaa muswada huo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa bunge maalumu la katiba yenye  wajumbe wanaojumuisha wabunge wote na wawakilishi wote wa baraza la wawakilishi kutoka Tanzania Visiwani.

Naye Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA) Bi.Ananilea Nkya, alisema kutolewe muda wa kutosha kwa wananchi kupata muswada na kujadili kabla ya kuwasilishwa kwa majadiliano rasmi bungeni.

Kwa mujibu wa serikali baada ya bunge kujadili na kupitisha muswada huo wa sheria tume maalum itaundwa na Rais Kikwete kwa kushauri na Rais wa Tanzania Visiwani na Mwansheria Mkuu wa serikali. Tume hiyo inatarajiwa kujumuisha makundi yote ya jamii.

Tume hiyo ndiyo itayotembea nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya wanayoitaka. Kazi ya uundwaji Katiba Mpya unatarajiwa kukamika mwaka 2014 hku vipengele vinavyoonekana kuwekewa mkazo zaidi ni madaraka ya Rais na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment