WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, anaendelea kufanyiwa mazoezi ya bega kwenye Taasisi ya Mifupa Muhimbi (Moi), baada ya kufanyiwa upasuaji hivi karibuni ameitaka Serikali kuisaidia Hospitali ya Taifa Muhimbili ili itoe huduma nzuri zaidi kwa wananchi.
Sumaye ambaye alifanyiwa upasuaji baada ya kuanguka na kusababishia maumivu upande wa kushoto wa bega, alisema Serikali lazima itazame Moi kwa upana zaidi, maana ndicho kituo pekee wanachotegemea wananchi kwa huduma za upasuaji na mifupa.
“Hapa ndiyo tunategemea ili kupata huduma, kwa hiyo Serikali lazima ipatazame vizuri kwa kuweka miundo mbinu mizuri na kuongeza idadi ya wataalamu ili kuondoa usumbufu,” alisema Sumaye. Pia, Sumaye alisema idadi ya wagonjwa katika hospitali hiyo imekuwa kubwa, hivyo hata huduma zimekuwa hafifu kwa upande mwingine maana wataalamu wamekuwa wadogo ukilinganisha na idadi ya wagonjwa.
“Unajua idadi inavyokuwa kubwa halafu wataalamu wakawa wadogo hapo ndipo huduma inapoonekana hafifu, kwa hiyo Serikali iongeze idadi ya wataalamu katika kituo hiki ambacho kinahudumia Watanzania wengi,” alisema Sumaye. Sumaye alisema suala la viongozi wengi kwenda nje ya nchi kutibiwa, inategemea huduma ambayo inahitajika kwa kiongozi huyo kama inapatikana nchini.
“Suala la viongozi kwenda nje ya nchi kutibiwa inategemea na huduma ambayo unaitaka, huwezi kwenda huko moja kwa moja bila kupewa ruhusa na madaktari wa hapa,” alisema Sumaye. Amekuwa akipata huduma ya mazoezi ya bega taasisi ya Moi kwa zaidi ya mwezi sasa.
Wakati huohuo, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, imeitaka Serikali kuanzisha hospitali za magonjwa ya mifupa kila mkoa, ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi). Mwenyekiti wa kamati hiyo, Margreth Sitta, alisema wamesikitishwa na msongamano wa wagonjwa katika taasisi ya Moi, unaofanya baadhi yao kulala sakafuni. "Kuna haja Serikali kuangalia tatizo hili na kulitafutia ufumbuzi harakati, hii ni shida," alisema Sitta. Sitta alisema hayo wakati kamati hiyo ilipotembelea taasisi hiyo na baadaye kuzungumza na wafanyakazi.
“Tumejionea wenyewe wagonjwa wanalala chini, tatizo ni vitanda na wanahitaji huduma kwa hiyo huwezi kumrudisha nyumbani ili asubiri kitanda kwa hiyo lazima Serikali itazame suala hili,” alisema. Mkuu wa Moi, Profesa Paul Mseru, alisema kitengo hicho kilianzishwa mwaka 1996 kwa malengo ya kutoa huduma kwa matatizo ya mifupa na upasuaji.
Pia, Profesa Mseru alisema kitengo hicho kina zaidi ya vitanda 180, lakini kinapokea idadi kubwa kupita uwezo wake, ndiyo maana wagonjwa wengine wanalala chini na kuomba Serikali kujenga kitengo kingine cha mifupa. “Tunaomba Serikali kufanya utaratibu wa kutoa huduma ya upasuaji kwa mikoa mingine, ili tupunguze msongamano ambao unajitokeza hapa,” alisema Profesa Mseru.
Sitta alisema lazima suala la kutoa huduma ya mifupa na upasuaji kwa mikoa mingine lifanywe haraka kutoa usumbufu kwa wagonjwa wanaolala chini. “Kwakweli ombi hili lazima lifike kwa Serikali na tutaomba ifanyie kazi haraka suala hili, maana idadi ya wagonjwa inatisha na hatari pia kwa wagonjwa kulala chini,” alisema Sitta. Wagonjwa ambao walikuwa wakisubiri huduma, walisema kupata huduma ni vigumu kwa sababu ya wingi wao ambao wanatoka mikoa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment