MADAKTARI wa Hospitali ya Apollo India, wamefanikiwa kumfanyia operesheni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ambaye alipelekwa huko wiki iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kipanda uso.
Kaka wa Mbunge huyo, Salum Mohammed aliliambia gazeti hili jana kuwa operesheni hiyo iliyotumia muda wa saa nne, ilifanyika salama na hali yake inaendelea vizuri. “Walianza kumfanyia operesheni saa 4:00 asubuhi na ilikamilika kwenye saa 8:00 mchana. Kwa sasa (Zitto) anaendelea vizuri.
Tayari amezinduka, amekunywa juisi na sasa (jana) amepumzika,” alisema Mohammed. Alisema operesheni ilifanywa na jopo la madaktari lililoongozwa na Dk Sunil Narayan Dutt ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya kinywa, njia ya kupumua na kichwa na pia ndiye mkuu wa kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya Appolo. Mohammed alisema madaktari hao walieleza kwamba aina ya operesheni hiyo huwa haihusishi upasuaji wa fuvu.
“Walichokifanya ni kuingiza chombo maalumu puani na kwa kutumia kompyuta, waliweza kuona kila kitu na ndipo wakaanza kufanya operesheni kwa kuona kupitia kompyuta,” alisema Mohammed. Alisema operesheni ilifanyika kikamilifu na Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema anaendelea vizuri na hakuna tatizo lolote ambalo linamsibu kutokana na upasuaji huo.
“Hadi sasa anaendelea vizuri na hakuna tatizo lolote ambalo limempata kutokana na upasuaji huo. Mheshimiwa Zitto anaendelea vizuri ingawa anaonekana kuchoka kutokana na shughuli hiyo,” alisema Mohammed. Zitto alipelekwa India kwa matibabu baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) iliyokuwa ikimpatia matibabu kupendekeza rufaa hiyo. Alipelekwa MNH akitokea katika Hospitali ya Aga Khan ya Dar es Salaam akitibiwa ugonjwa wa malaria.
Zitto ambaye amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kipanda uso kwa miaka 10 sasa, Jumatatu wiki hii aliliambia gazeti hili kwamba hali yake imeimarika zaidi baada ya kupelekwa kwenye hospitali hiyo iliyoko katika Jiji la Bangalore.
Katika kipindi hicho cha muongo mmoja, Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni alisema alipoteza fahamu na kuanguka mara nne tofauti.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2000 akiwa Mwanza wakati akielekea kwenye Mkutano wa Vijana wa National Youth Forum na mara ya pili ilikuwa Mjini Dodoma katika mkutano kama huo mwaka 2001, usiku.
Mara ya tatu anasema alikuwa chumbani Hall II, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2002 wakati huo akiwa mwanafunzi mara baada ya kutoka kujisomea jioni.
Zitto alisema mara ya nne hali hiyo ilimtokea akiwa bungeni siku ya kupitisha Muswada wa Madini 2010 akisema hiyo ilitokana na kuwa katika hekaheka ya wiki nzima ya vikao vya Kamati na Mjadala wa Bunge.
Alisema tatizo lililomfikisha India lilianza Ijumaa ya Oktoba 20, mwaka huu Dar es Salaam mara baada ya kuwasili kutoka jimboni tayari kwa kazi za Kamati za Bunge akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).
No comments:
Post a Comment